Mtaalamu
wa maridhiano na utatuzi wa migogoro, Dkt. Dennis Mchunguzi, ameisifu
Tume ya Uchunguzi iliyoongozwa na Mohamed Othman Chande kwa
kutekeleza jukumu lake kwa mafanikio ndani ya siku 153, akibainisha
kuwa kazi hiyo ilihitaji kiwango cha juu cha umakini, weledi na
uzalendo.
Pia alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi
wa kuunda tume hiyo, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha nia ya dhati
ya Serikali katika kutafuta ukweli na kuimarisha misingi ya haki
pamoja na amani nchini.
Akizungumza baada ya kuisoma ripoti
hiyo, Dkt. Mchunguzi alisema imeandaliwa kwa ustadi mkubwa wa
kitaaluma, ikizingatia viwango vinavyotakiwa na kutekeleza kikamilifu
hadidu za rejea zilizopewa tume hiyo.
Hata hivyo, alieleza
masikitiko yake kufuatia madhara yaliyosababishwa na vurugu za Oktoba
29, zikiwemo vifo vya watu, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali,
akisisitiza kuwa matukio hayo yameacha athari kubwa kwa jamii na
taifa kwa ujumla.
Alijiunga na Rais Samia kutoa pole kwa
familia zilizopoteza wapendwa wao na wale walioathirika kwa namna
mbalimbali, akihimiza mshikamano wa kitaifa katika kipindi
hiki.
Aidha, alibainisha kuwa ripoti hiyo ni nyenzo muhimu
katika kujenga msingi imara wa haki, uwajibikaji na maridhiano ya
kweli, ambayo ni muhimu kwa mustakabali wa nchi.
Alisisitiza
pia umuhimu wa kudumisha umoja wa kitaifa na kuchukua tahadhari dhidi
ya vitendo au mienendo inayoweza kuhatarisha maendeleo ya taifa.
#UmojaWetuNdiyoNguvuYetu
#turidhiane

0 Maoni