Viongozi washtushwa na mkasa wa risasi Marekani

 

Viongozi kutoka kote ulimwenguni wameelezea mshtuko pamoja na faraja kwa kukamatwa mtu anayeshukiwa kufyatua risasi kwenye hafla ya chakula cha jioni iliyohudhuriwa na Rais wa Marekani Donald Trump mjini Washington.

Milio ya risasi ilisikika wakati wa hafla hiyo ya kila mwaka ya waandishi habari wa Ikulu ilipokuwa ikifanyika katika hoteli ya Washington Hilton Jumamosi jioni, na kusababisha vikosi vya usalama kuwaondoa haraka Trump, mkewe Melania, Makamu wa Rais JD Vance na maafisa wengine wakuu kutoka ukumbini.

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema ni faraja kubwa kwamba rais, mke wa rais na wote waliohudhuria wako salama. Aliongeza kwa kusema kuwa shambulio lolote dhidi ya taasisi za kidemokrasia au uhuru wa vyombo vya habari lazima lilaaniwe kwa nguvu zote.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameelezea shambulio hilo kuwa lisilokubalika, huku Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen akisema kwamba ghasia hazina nafasi kamwe katika siasa.

Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu, mshirika wa karibu wa Trump, naye amesema yeye na mkewe wameshtushwa na jaribio la kumuua Trump.

Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney, pia alielezea faraja kwamba kila mtu aliyehudhuria yuko salama. Alisema machafuko ya kisiasa hayana nafasi katika demokrasia yoyote. Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum pia aliandika kwenye mtandao wa X kwamba "Ghasia hazipaswi kamwe kuwa jibu."

Chapisha Maoni

0 Maoni