Wakati siku zikisalia chache kabla ya Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani kuwasilisha ripoti yake, wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wameelezea matumaini makubwa kuwa majibu yatakayotolewa yatagusia matamanio ya dhati ya Watanzania.
Tume hiyo, inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, inatarajiwa kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ifikapo au kabla ya Aprili 3, 2026, baada ya kuongezewa muda wa siku 42 tangu Februari mwaka huu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Paul Loisulie, amesisitiza kuwa wajumbe walioteuliwa kuunda tume hiyo wana weledi wa kutosha na uzoefu uliotukuka. Kauli hiyo imeungwa mkono na Dk. Richard Mbunda wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyebainisha kuwa sifa na uwezo wa Jaji Chande na timu yake si wa kutiliwa shaka.
“Imani yetu ni kwamba ripoti hii itawaondoa hofu Watanzania kwa kuwasilisha kitu tofauti na hisia zinazozungumzwa mitaani kwa sasa. Kila kitu kinategemea utayari wa tume kufunguka na kuja na ukweli utakaokidhi matarajio ya wananchi,” alisema Dk. Mbunda.
Licha ya imani hiyo, Dk. Mbunda ameibua hoja ya kisheria akibainisha kuwa uamuzi wa ripoti hiyo kuwekwa hadharani unabaki kuwa mikononi mwa Rais. Ingawa sheria inampa Rais mamlaka ya kuzuia au kutoa ripoti hiyo kwa umma, wachambuzi wanaona kuwa kuiweka wazi kutaongeza imani ya wananchi kwa serikali na taasisi zake.
Mjumbe mstaafu wa Halmashauri Kuu ya CCM (MNEC) Taifa, Lucas Millasi, amewahimiza Watanzania kuwa na imani na tume hiyo kutokana na rekodi za kiutumishi za wajumbe wake. Millasi aliwataja wajumbe kama Balozi Ombeni Sefue (Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu) na Said Mwema (IGP mstaafu) kama watu "wasafi" walioitumikia nchi kwa heshima bila madoa ya kimaadili.
“Rais Samia hakuridhika na yaliyotokea Oktoba mwaka jana, ndiyo maana akatafuta watu makini. Nia yake ni kupata suluhisho la kudumu, si majibu mepesi. Jaji Chande amewahi kuongoza tume za uchunguzi wa mauaji huko nyuma, hivyo anajua umuhimu wa jukumu hili kwa mustakabali wa demokrasia yetu,” alisema Millasi.
Wachambuzi hao wamefananisha Tume ya Jaji Chande na tume zilizowahi kuacha alama nchini, kama ile ya Jaji Kisanga na Jaji Francis Nyalali, ambazo zilikuja na mapendekezo yaliyobadili mwelekeo wa nchi.
Inatarajiwa kuwa ripoti hii itatibu chanzo cha matatizo ya uchaguzi na kutoa dira ya nini kifanyike ili matukio ya uvunjifu wa amani yasijirudie tena, huku ikijenga msingi imara wa utawala bora na demokrasia inayoweza kuigwa na mataifa mengine.
Tume hiyo inayofanya kazi chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi (Sura ya 32), sasa iko katika hatua za mwisho za kukamilisha maandishi yake tayari kwa makabidhiano ya kihistoria yatakayoamua hatma ya utulivu wa kisiasa nchini.

0 Maoni