Makaa ya mawe kuchochea maendeleo ya viwanda nchini Tanzania

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema makaa ya mawe yana nafasi ya kimkakati katika kuharakisha mageuzi ya uchumi wa Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda, akibainisha kuwa rasilimali hiyo si tu chanzo cha nishati bali pia ni mhimili wa kuongeza thamani ya madini na malighafi nyingine za viwandani. Amesema kupitia matumizi sahihi ya makaa ya mawe, nchi inaweza kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje, kuongeza uzalishaji wa ndani na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta mbalimbali ikiwemo  nishati, viwanda na madini.

Akizungumza leo Machi 30, 2026 katika kikao na wadau wa makaa ya mawe kilichofanyika katika Ukumbi wa Tume ya Madini, Jijini Dodoma, Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wadau ili kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa kasi na ufanisi zaidi.

“Makaa ya mawe ni mhimili muhimu katika maendeleo ya viwanda. Tunahitaji kuongeza uzalishaji na kuhakikisha matumizi yake yanaongeza thamani ndani ya nchi,” ameeleza Mhe. Mavunde.

lKatika kikao hicho, Waziri Mavunde amepokea changamoto mbalimbali kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara, ikiwemo gharama za uzalishaji, usafirishaji na upatikanaji wa masoko na kuahidi kuwa Serikali itazifanyia kazi ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Aidha, amesisitiza kuwa upangaji wa bei elekezi utafanyika kwa ushirikishwaji wa wadau wote ili kulinda maslahi ya sekta.

Wadau wa makaa ya mawe wameipongeza hatua hio ya Waziri Mavunde na kueleza kuwa Serikali kwa kuwashirikisha katika majadiliano, wakieleza kuwa hatua hiyo imeongeza imani na uwazi katika uendeshaji wa sekta hiyo huku wakiahidi kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe ili kukidhi mahitaji ya ndani na kuongeza mapato ya Taifa kupitia Sekta ya Madini.

Katika kuimarisha uratibu na mshikamano wa sekta, Mhe. Mavunde amewahimiza wadau wa makaa ya mawe kuanzisha chama chao (association) kitakachowaunganisha ili kurahisisha shughuli zao na kushughulikia changamoto kwa pamoja kwa ufanisi zaidi.

Katika hatua ya kuimarisha viwanda vya ndani, Waziri Mavunde amesema kuwa Kampuni ya A1 Steels Tanzania LTD imepanga kujenga Kiwanda cha kuzalisha chuma jijini Dodoma na kwamba kiwanda hicho kinatarajiwa kutumia takribani tani 20,000 za makaa ya mawe kwa mwaka, hatua inayotarajiwa kuongeza mahitaji ya rasilimali hiyo na kufungua fursa zaidi za uzalishaji kwa wachimbaji wa ndani.

Mradi huo unatarajiwa kuchochea ajira, kuongeza thamani ya madini na kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa.

Kikao hicho kimeonesha dhamira ya Serikali ya kuifanya Sekta ndogo ya makaa ya mawe kuwa injini ya maendeleo ya viwanda nchini, huku ushirikiano kati ya Serikali na wadau ukiendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya sekta hiyo.





Chapisha Maoni

0 Maoni