Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amezuru eneo la ujenzi wa
Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro Januari 02 mwaka 2026 na kutoa agizo zito kwa
Wizara ya Maji kuhakikisha mradi huo hausimami na unakamilika kwa wakati uliopangwa
ili uanze kutoa huduma kwa wananchi.
Katika ziara hiyo Waziri Mkuu ameiagiza wizara husika
kuandaa jedwali maalumu litakalokuwa mwongozo wa kasi kwa mkandarasi katika
utekelezaji wa mradi huo huku akisisitiza kuwa ujenzi huu unaakisi maono ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji
nchini.
Dkt. Mwigulu amebainisha kuwa Rais Samia ni kiongozi
anayeona mbali kwani aliamua kutekeleza mradi huu wa kimkakati katika kipindi
ambacho serikali inatekeleza miradi mingine mikubwa inayotumia fedha nyingi
ikiwa ni hatua ya makusudi ya kutatua kero za Watanzania zinazotokana na
mabadiliko ya tabianchi.
Akifafanua faida za mradi huo utakaogharimu kiasi cha
shilingi bilioni 366, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema kuwa kukamilika kwa
bwawa hilo kutasaidia kuhifadhi lita bilioni 190 za maji zitakazokuwa mkombozi
mkubwa wakati wa ukame pale kina cha Mto Ruvu kinapopungua.
Waziri Aweso ameongeza kuwa mbali na huduma ya maji mradi
huo utazalisha takribani megawati 20 za umeme na utahusisha ujenzi wa barabara
yenye urefu wa kilometa 72 hatua itakayochochea maendeleo ya kijamii na
kiuchumi.
Naye Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo amechombeza neema
hiyo kwa kusema kuwa eneo kubwa linalozunguka bwawa hilo ni zuri kwa kilimo na
wizara yake imejipanga kuwezesha kilimo cha umwagiliaji kwa mwaka mzima ili
kukuza uzalishaji na malighafi za viwandani.
Safari hii ya miongo saba ya kiu na matumaini sasa inafikia
tamati baada ya miaka mingi ya kusubiri huku kero ya mgao wa maji ikitesa
wakazi wa Dar es Salaam na Pwani .
Mradi huu wa kihistoria uliokuwa ndoto tangu miaka ya
hamsini wakati wa serikali ya kikoloni sasa unatekelezwa kama alama ya ushindi
dhidi ya changamoto za kimazingira zilizokuwa zimekwamisha mchakato huo kwa
miaka mingi.
Kidunda itakuwa na uwezo wa kusambaza zaidi ya lita milioni
400 za maji kwa siku jambo litakalofanya kero ya mgao kubaki kuwa historia na
kuleta utulivu kwa akina mama na familia zilizokuwa zikiteseka kutafuta huduma
hiyo muhimu mjini na vijijini.
Mchanganuo wa mradi huu unaonyesha historia ndefu ambapo
michoro ya awali na upembuzi yakinifu ulianza kufanyika zaidi katika miaka ya
themanini kwa lengo la kudhibiti mafuriko na kutengeneza akiba ya maji ya
kiangazi.
Mradi huu ulichelewa kwa miongo kadhaa kutokana na sababu
kuu tatu ikiwemo mgogoro wa kimazingira na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu
, sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kwani eneo la mradi
linapakana na Pori la Akiba la Selous ambalo sasa ni Hifadhi ya Taifa ya
Nyerere. Sababu nyingine ilikuwa ni mabadiliko ya michoro mara kwa mara ili
kuridhisha wadau wa mazingira pamoja na changamoto za kifedha ambazo sasa
zimetatuliwa na serikali ya awamu ya sita iliyoamua kuupa mradi huu kipaumbele
kwa fedha za ndani.
Shinikizo kubwa la kuhimiza kasi ya ujenzi hivi sasa
linatokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha mto Ruvu kukauka
mara kwa mara pamoja na ongezeko kubwa la watu na viwanda katika jiji la Dar es
Salaam. Bila bwawa hili ukuaji wa viwanda na makazi unaathirika vibaya : na ndiyo
maana agizo la Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba limekuja wakati muafaka kuzuia
mradi usirudi tena kwenye usingizi wa miaka ya nyuma.
Hakika huu ni wakati wa neema ambapo kila tone la maji
litakalotoka Kidunda litakuwa ni ushahidi wa kazi kubwa ya serikali katika
kumkomboa mwananchi na kuliimarisha taifa kiuchumi na kijamii kwa viwango vya
kimataifa huku kila upande ukijipanga kunufaika na uwekezaji huo wa Sh bilioni
366.

0 Maoni