Kadiri
siku zinavyosogea kuelekea kilele cha sikukuu za mwisho wa mwaka, imebainika
wazi kuwa "vidonge" vya uzalendo na amani vimeanza kuwakolea wale
wote wenye nia ovu ya kutaka kuivuruga nchi. Watanzania, kwa ukomavu wao wa
hali ya juu, wameendelea kuonesha kuwa wanazijua janja za wachochezi wanaotaka
kuiunguza nchi kwa maslahi yao binafsi na ya mabeberu.
Msimamo
huu wa wananchi umekuwa pigo kubwa kwa makundi yanayojaribu kuhamasisha vurugu,
kwani kama ambavyo watanzania hawakushiriki "ujinga" uliopangwa
Desemba 9 , ndivyo ambavyo Desemba 25 itapita kwa amani na utulivu. Ujumbe
umefika: Tanzania si uwanja wa majaribio ya fujo.
Katika
kuunga mkono misingi ya nchi, kauli ya mzee maarufu na mshauri wa masuala ya
uongozi, Mzee Joseph Butiku, imetoa mwelekeo chanya. Mzee Butiku amesisitiza
kuwa Rais ameshachaguliwa na ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, si
Rais wa chama fulani pekee. Ni nguzo ya taifa na ni wajibu wa kila mzalendo
kumlinda na kumheshimu kwa sababu anawakilisha utu na mamlaka ya nchi yetu.
Wale
wanaopiga kelele wakitaka Rais "aondoke kesho" wanajidanganya.
Watanzania hawajafanya kosa kumchagua kiongozi wao, na jitihada zozote za
kutaka kumuondoa nje ya taratibu za kisheria na kikatiba hazitakubalika na hazitapata
mwitikio wa umma. Tunazungumza juu ya Rais wetu kwa nia njema, kwa heshima, na
kwa kuthamini kazi anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Licha
ya kuwepo kwa maoni mseto kwenye mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya watu
wanajaribu kumshambulia Mzee Butiku kwa kauli yake ya kishujaa, ukweli unabaki
palepale: busara za wazee ndizo zinazolivusha taifa hili kwenye dhoruba.
Mashambulizi dhidi ya wazee wanaosimamia ukweli ni ishara ya kukata tamaa kwa
wale ambao mipango yao ya vurugu imefeli.
Wanaodai
kuwa uchaguzi uliibiwa au Rais hatakiwi, ni kundi lilelile ambalo limekuwa
likitumiwa kama vibaraka wa maslahi ya nje. Watanzania wa leo si "bendera
fata upepo"; wanajua kutofautisha kati ya ukosoaji wenye tija na uhaini
unaolenga kubomoa misingi ya amani tuliyoirithi kutoka kwa waasisi wa taifa
hili.
Tunapoelekea
mwishoni mwa mwaka, kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzake. Tuwapuuze
wale wote wanaotumia lugha za kuudhi na uchochezi kwenye majukwaa ya
kidijitali. Tunapaswa kukumbuka kuwa amani ikitoweka, hakuna atakayebaki
salama—iwe mfuasi wa serikali au mpinzani.
Rais
wetu ni alama ya umoja wetu. Hatukubali na hatutakubali kuyumbishwa na bahasha
za mabeberu au ahadi za uongo kutoka kwa watu wasioitakia mema Tanzania.
Desemba 25 itakuwa siku ya furaha, amani, na shukrani, na si siku ya kushiriki
"miradi ya giza" ya watu wachache wenye njaa ya madaraka.

0 Maoni