Viongozi wa kijamii, kidini, na kisekta wametoa wito mzito
kwa Watanzania wote kudumisha amani na utulivu kama msingi mkuu wa kusukuma
mbele gurudumu la maendeleo mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha uchaguzi
mkuu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamesisitiza
kuwa umoja wa kitaifa ndiyo siri ya mafanikio ya Tanzania.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania
(JMAT) Wilaya ya Mkuranga, Shukuru Ngweshani, ameeleza kuwa ili kudumisha
amani, Watanzania wanapaswa kuaminiana bila kubaguana.
"Ili tudumishe amani tunapaswa kuaminiana bila
kubaguana kwani watu watakaa pamoja na kufanya shughuli za maendeleo kwa
pamoja. Utulivu na mshikamano ndiyo jadi ya nchi yetu, tushirikiane katika
kuleta maendeleo," alisisitiza Ngweshani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa African Talent Forum (ATF),
Rosemary Bujashi, amewataka wananchi kuitazama amani kama ngao kuu ya kujilinda
dhidi ya watu wasioitakia mema nchi yetu. Amehimiza Watanzania kupuuza sauti za
wale wanaojaribu kuwagawa.
"Amani ni ngao ya nchi yetu, tunapaswa kuitumia ili
kujilinda na wale wasioitakia mema nchi yetu. Tuilinde amani kwa gharama
yoyote. Tudumishe mshikamano wetu katika kujiletea maendeleo ya nchi yetu na
tuachane na wale wanaotaka kutugawa," alisema Bujashi.
Naye Diwani wa Kata ya Mkuranga, Hamza Mahanaka, ametoa
ujumbe mahususi kwa vijana akitaka waepuke makundi yanayoweza kuyumbisha uchumi
na kurudisha nyuma juhudi za maendeleo. Amesema kuwa utulivu unatoa fursa kwa
viongozi na wananchi kufanya kazi bila hofu huku ukivutia wawekezaji.
"Vijana tudumishe amani na kuachana na makundi ambayo
yanarudisha nyuma juhudi za maendeleo na kuyumbisha nchi kiuchumi. Viongozi
wahubiri upendo na mshikamano kuvutia wawekezaji...tuongeze mshikamano ili
tuweze kujiletea maendeleo ya nchi yetu," alieleza Mahanaka.
Viongozi hawa wote wanagusia jambo moja kuu: Amani ya
Tanzania ni tunu inayopaswa kulindwa na kila mzalendo. Baada ya uchaguzi, kazi
iliyobaki ni moja tu kushirikiana kama taifa moja kuelekea maendeleo ya
kiuchumi na kijamii.

0 Maoni