Katika kile kinachoonekana kama operesheni ya kuimarisha
ulinzi wa Taifa kuanzia ngazi ya kaya, viongozi wa Serikali za Mitaa na wadau
wa usalama nchini wametoa onyo kali kwa wamiliki wa nyumba wanaokubali
kuhifadhi wageni wasiojulikana kwa tamaa ya fedha. Onyo hilo linakuja huku
kukiwa na hofu kuwa makazi ya watu yanageuzwa kuwa "vyumba vya siri"
(safe houses) kwa ajili ya kupanga njama za kihalifu na hujuma dhidi ya taswira
ya Tanzania.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Magole, Ilala, Gaddafi
Hassani, akizungumza kwa niaba ya mtazamo mpana wa kiusalama, amesema kuwa
ulinzi wa nchi si jukumu la vyombo vya dola pekee, bali unaanza na umakini wa
mwenye nyumba anayempa ufunguo mtu asiyemjua.
Fedha ya Kodi dhidi ya Usaliti wa Taifa
Mwenyekiti Hassani amefichua mbinu mpya inayotumiwa na watu
wenye nia ovu, wakiwemo wahalifu wa kuvuka mipaka na wachochezi wa machafuko.
Amesema watu hao hupanga nyumba katika vitongoji tulivu, wakitoa kiasi kikubwa
cha fedha ili "kununua" ukimya wa mwenye nyumba na kukwepa taratibu
za kusajiliwa serikali za mitaa.
"Usikubali kumpa hifadhi mtu anayekupa mamilioni ya
kodi lakini hataki kutoa kitambulisho wala kufika ofisi ya mtaa. Kwa kufanya
hivyo, unajenga 'chimbo' la kuisaliti nchi yako. Fedha hizo ni za muda, lakini
majanga ya kiusalama yakitokea, yataigharimu nchi nzima ikiwemo familia
yako," alisisitiza kiongozi huyo.
Tanzania ni yetu sote. Usikubali "kuchuuzwa" kwa
fedha kidogo za kodi ambazo mwisho wake ni kuingiza Taifa kwenye majanga.
Uzalendo ni kumlinda jirani yako, mtaa wako, na nchi yako kwa kutomfuga adui
ndani ya nyumba yako.
Ugeni kama Kivuli cha Uhujumu
Inabainika kuwa mwishoni mwa mwaka, kuna ongezeko la watu
wanaohama kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine au kuingia nchini kwa kivuli cha
biashara na utalii, lakini lengo likiwa ni kutafuta ramani za uhalifu. Serikali
imebaini kuwa baadhi ya wageni hawa hutumika na mitandao ya kidhalimu inayotaka
kuchafua taswira ya Tanzania kama kisiwa cha amani.
Wito wa
"Uzalendo wa Taarifa"
Mjumbe wa Nyumba 10, Edwin Wandawanda, amesema kuwa kila
mwananchi anapaswa kuwa "Afisa Usalama wa Nyumba Yake". Alisisitiza
kuwa ni lazima jamii ijifunze kuwa na kutilia shaka (positive skepticism) kwa
wageni wanaokuja na mitindo ya maisha isiyoeleweka.
"Tunapaswa kuelewa kuwa amani yetu inategemea usiri na
umakini wetu. Ukiona mtu amepanga nyumbani kwako, hatoki mchana, ana wageni wa
ajabu usiku, na hataki kujihusisha na jamii, huyo ni hatari kwa usalama wa
Taifa. Toa taarifa mara moja," alisema Wandawanda.
Hatua za Kimkakati Kitaifa
Kufuatia hali hiyo, mamlaka za mitaa zimeelekezwa
kushirikiana na Polisi Jamii kuhakikisha:
Uhakiki wa NIDA: Hakuna mpangaji anayeruhusiwa kuingia
nyumbani bila namba au kitambulisho cha NIDA au Pasipoti halali kwa wageni.
Daftari la Wakazi: Kila mwenye nyumba ana wajibu wa
kisheria kusajili wapangaji wake kwenye daftari la kijiji au mtaa.
Kufuta "Vyumba vya Siri": Nyumba yoyote
itakayogundulika kuhifadhi wahalifu au watu wanaopanga njama dhidi ya nchi,
mmiliki wake atachukuliwa kama mshiriki wa uovu huo (accomplice).

0 Maoni