Mwenyekiti TBN Awapongeza Watanzania, Atoa Wito wa Umoja Kuelekea 2026

 

Tunapouaga rasmi mwaka 2025, Mwenyekiti wa Tanzania Bloggers Network (TBN), Beda Msimbe, amewapongeza Watanzania wote kwa kumaliza mwaka huo kwa uthabiti, moyo wa kizalendo na mshikamano, akieleza kuwa umekuwa mwaka wenye matukio mengi ya kihistoria kwa Taifa.

Akitoa salamu za mwaka mpya kwa niaba ya wanachama wote wa TBN, Msimbe amewashukuru wasomaji na wadau mbalimbali kwa kuendelea kufuatilia habari, uchambuzi na taarifa kupitia majukwaa ya kidijitali ya mtandao huo, akisisitiza kuwa mchango wao umekuwa nguzo muhimu katika kukuza tasnia ya habari za mtandaoni nchini.

“Kupitia ushiriki wenu, TBN imeendelea kuwa sauti ya wananchi na jukwaa huru la mijadala yenye tija kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Msimbe.

Mageuzi Makubwa 2026

Akizungumzia matarajio ya Mwaka Mpya 2026, Mwenyekiti huyo amesema TBN imejipanga kuleta mageuzi makubwa yatakayolenga kuboresha ubora wa maudhui, kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kisasa, pamoja na kuwasilisha habari za kina zitakazosaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi.

Ameeleza kuwa wanachama wa TBN wataendelea kuwa daraja imara kati ya serikali na wananchi kwa kuhakikisha habari sahihi, za kuaminika na kwa wakati zinafika kwa kila Mtanzania, mijini na vijijini.

Wito wa Amani na Umoja

Katika salamu zake za Mwaka Mpya, Msimbe ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, akisisitiza umuhimu wa kuepuka migawanyiko na vurugu zisizo na tija.

“Huu ni wakati wa kuungana kwa nguvu moja ili kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na maendeleo ya kweli na anapata sehemu yake ya ‘keki ya taifa’,” amesema.

Ujumbe wa Heri ya Mwaka Mpya

Akihitimisha ujumbe wake, Mwenyekiti wa TBN amewaombea Watanzania mwaka 2026 uwe mwaka wa neema, baraka na mafanikio tele katika kazi na shughuli zao za kila siku.

“Heri ya Mwaka Mpya 2026 kwa Watanzania wote,” amehitimisha Msimbe.

Chapisha Maoni

0 Maoni