Tunapoelekea mwaka 2030, Tanzania inatarajiwa kushuhudia
mapinduzi makubwa ya kiuchumi ambayo msingi wake umewekwa katika kipindi hiki
cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ramani hii ya mafanikio haitegemei bahati, bali inategemea
kukamilika kwa miradi ya kimkakati ambayo kwa sasa inatoa jasho na rasilimali
nyingi za taifa. Ikiwa amani itadumu na mipango ya sasa ikatekelezwa bila
kuingiliwa na vurugu za kisiasa, ifikapo mwaka 2030 maisha ya kijana wa
Kitanzania yatakuwa na sura mpya kabisa.
Kukamilika kwa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa na ununuzi wa meli
tano kubwa za uvuvi ni mwanzo wa safari. Ifikapo mwaka 2030, mnyororo wa
thamani wa sekta ya uvuvi unatarajiwa kuwa na viwanda vya uchakataji samaki
kando kando ya mwambao wa bahari ya Hindi na maziwa makuu.
Hii inamaanisha kuwa kijana wa mwaka 2030 hatakuwa
anatafuta kazi ya ukarani tu, bali atakuwa mmiliki wa viwanda vidogo vya
vifungashio, mtoa huduma za usafirishaji (logistics), na mtaalamu wa teknolojia
ya kisasa ya uvuvi.
Bandari ya Kilwa pekee inategemewa kuchochea ajira za moja
kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa watu zaidi ya 30,000, likiwa ni kundi
kubwa la vijana.
Gridi ya Taifa ya Maji na kukamilika kwa miradi mikubwa ya
umeme kama Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) kutaifanya Tanzania kuwa na nishati
ya uhakika na ya bei nafuu.
Mwaka 2030 unatarajiwa kuwa mwaka ambao kijana wa vijijini
anaweza kuanzisha karakana ya kulehemu, kiwanda cha kusaga nafaka, au biashara
ya saluni bila hofu ya kukatika kwa umeme au ukosefu wa maji safi. Uhakika wa
huduma hizi utapunguza gharama za uendeshaji biashara (Cost of Doing Business),
jambo ambalo litaongeza faida kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs) na
kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
Barabara kuu kama ile ya Marendego – Lindi na uboresha wa
reli ya kisasa (SGR) vinaunganisha Tanzania na masoko ya nchi jirani kama
Zambia, DRC, na Malawi. Ifikapo mwaka 2030, kijana wa Tanzania atakuwa na uwezo
wa kusafirisha bidhaa zake kutoka viwanda vya ndani kwenda nchi yoyote ya
jirani kwa gharama nafuu na muda mfupi. Hii inafungua fursa ya
"Cross-border Trade" ambapo vijana watakuwa mawakala wa biashara za
kimataifa, wakitumia bandari zetu zilizoboreshwa kama lango kuu la biashara
barani Afrika.
Ramani hii ya mafanikio inaweza kutimia tu ikiwa kila tone
la rasilimali litatumika kwa maendeleo badala ya kurudia michakato ya kisiasa
isiyo na tija.
Mwaka 2030 utakuwa ni mwaka wa mavuno kwa wale
waliojituliza na kuwekeza nguvu zao kwenye miradi na ubunifu badala ya kufuata
kelele za wachochezi. Rais Dkt. Samia ameshaonesha njia; ni jukumu la kila
kijana mzalendo kulinda amani ya sasa ili kuhakikisha kuwa safari hii ya
kuelekea 2030 haikwami njiani. Tanzania ya kesho ni ya wale wanaoijenga leo kwa
mikono yao na akili zao.

0 Maoni