Jeshi la Polisi
nchini Tanzania limetoa wito kwa wananchi wote kwa nafasi zote kuanzia ngazi ya
familia kuwakataa watu wanaohamasisha uvunjifu wa amani na sheria kwani malengo
yao ni kuharibu Taifa na kuwarudisha watanzania kwenye machungu ya Oktoba 29, 2025.
Aidha limesema kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na usalama linaendelea kufuatilia kwa
karibu yanayoendelea kwenye Mitandao ya Kijamii na kwenye makundi sogozi.
Polisi pia imeeleza
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa linaendelea kuzuia uhalifu
sambamba na kuwakamata wale wanaofanya makosa mbalimbali ikiwemo ya Kimtandao
kwa wale wanaoendesha makundi mbalimbali katika Mitandao ya kijamii ya
kuhamasisha uhalifu na kuwachukulia hatua kulingana na sheria za nchi.
Msemaji wa Jeshi
la Polisi David Misime katika taarifa hiyo amelaani pia kile kinachoelezwa
katika makundi hayo ya mitandao ya Kijamii ikiwemo ya wito wa kutoshika silaha
katika maandamano hayo ikiwa mwandamanaji hakupitia mafunzo na badala yake
waachie silaha wenye mafunzo.
"Kupitia
Mitandao na Klabu mbalimbali za Mtandaoni wanahamasishana pia kusiwe na
shughuli nyingine itakayoendelea katika jamii. Pia wahakikishe wanaharibu na
kuchoma moto minara yote ya mawasiliano ili nchi nzima ikose mawasiliano,
wanahamasishana pia wahakikishe bandari ya Dar Es Salaam haifanyi kazi kwani
watafunga barabara zote zinazoingia na kutoka Bandarini na zile
zinazoiunganisha Tanzania na nchi za jirani." Amesema Misime.
Aidha,
waandamanaji hao pia wanahamasishana kuwafuata popote walipo watumishi wa
serikali ili kuwadhuru.

0 Maoni