Kilele cha utambuzi wa uandishi wa habari za kidijitali nchini Tanzania kimethibitishwa baada ya Bi. Veronica Mrema, Mwanzilishi wa chombo cha habari cha M24 TANZANIA MEDIA na mwanachama mahiri wa Tanzania Bloggers Network (TBN), kuingia rasmi kwenye jopo la mdahalo katika Mkutano wa 13 wa Kimataifa wa Waandishi wa Habari za Sayansi (WCSJ2025) unaofanyika jijini Pretoria.
Hili si tu fahari kwa Mrema binafsi, bali ni
heshima kubwa kwa TBN na tasnia nzima ya habari nchini, ikionesha kuwa kazi ya
uandishi wa kidijitali inatambulika katika majukwaa makuu duniani.
Mrema yuko Afrika Kusini kuhudhuria mkutano
huo mkuu unaotarajiwa kudumu hadi Desemba 5, 2025, baada ya kukabidhiwa
udhamini maalum wa safari (Travel Grant) na Wizara ya Sayansi, Teknolojia, na
Ubunifu ya Afrika Kusini (DSTI).
Udhamini huu ulikuja kama matunda ya utambuzi
wa utendaji wake wa kipekee katika uandishi wa habari za kisayansi na afya,
akibainishwa kuwa miongoni mwa wachache barani Afrika waliochaguliwa kwa
heshima hiyo. Uwepo wake kwenye jopo la mdahalo unampa fursa adhimu ya
kushiriki moja kwa moja katika kuunda mwelekeo wa mustakabali wa habari za
sayansi duniani.
Akiwa anahutubia jukwaa la WCSJ2025 ambalo
linakutanisha waandishi, watafiti, na wataalamu mashuhuri kutoka kote duniani,
Veronica Mrema anatarajiwa kusisitiza kuwa tasnia ya habari za sayansi na afya
barani Afrika inakua kwa kasi na kwa hivyo inahitaji sasa zaidi ya wakati
mwingine uandishi wa weledi wa hali ya juu, ubunifu, na ushahidi wa ki-sayansi
ili kufikisha ujumbe sahihi na wa kuaminika kwa jamii.
Lengo lake kuu ni kuhakikisha uelewa sahihi wa
sayansi unakuza maamuzi yanayoleta maendeleo, huku akitumia uzoefu wake kama
kiongozi, ikiwemo nafasi yake kama Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya
Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR-PC) na Afisa Habari wa Jumuiya
ya Watu Wanaoishi na Selimundu Tanzania (SCDPCT), kutetea uandishi wenye tija.
Kutambulika huku kwa Mwanachama wa TBN
kunaimarisha nafasi ya Tanzania katika uwanja wa uandishi wa habari za kisasa,
kuashiria kwamba mchango wake katika upashanaji habari ni wa kiwango cha
kimataifa.

0 Maoni