"Tanzania inaendelea kuwa mfano wa amani na
mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani kote."
Hayo ni maneno ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Mheshimiwa António Guterres, alipokuwa akipokea ujumbe maalumu kutoka kwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo.
Ujumbe huo uliwasilishwa na Mjumbe Maalum, Mheshimiwa
Balozi Mahmoud Kombo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Katibu Mkuu Guterres alitambua kuwa sifa ya Tanzania
kama nembo ya amani ilipimwa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 29
Oktoba 2025. Hata hivyo, alipongeza uthabiti wa nchi katika kudumisha umoja na
utulivu wa kitaifa.
Alisisitiza ni maslahi ya Umoja wa Mataifa kuiona
Tanzania ikiendelea kubaki imara na kutumika kama mfano chanya.
Katibu Mkuu huyo wa UN pia alisisitiza umuhimu wa
mazungumzo ya kitaifa yenye maana na jumuishi. Lengo la mazungumzo hayo ni
kushughulikia mizizi ya matukio ya vurugu yaliyotokea tarehe 29 Oktoba 2025, na
kuweka mikakati ya kuzuia kujirudia kwa matukio kama hayo.
Alihitimisha kwa kuthibitisha msaada kamili wa Umoja
wa Mataifa kwa jitihada zinazoendelea za Tanzania, ikiwemo kutoa msaada wakati
na baada ya kukamilika kwa kazi ya Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa nchini humo.

0 Maoni