Mchango wa amani ya kudumu katika ustawi wa kiuchumi na kijamii wa Tanzania umesisitizwa na wachambuzi na wananchi mbalimbali, wakitoa wito wa kuishi amani kwa matendo na kuimarisha uwajibikaji wa viongozi. Kauli hizi zimetolewa kufuatia mijadala kuhusu athari mbaya za vurugu zinazojitokeza wakati wa chaguzi barani Afrika.
Dkt.
Francis Daudi, mtaalamu wa masuala ya jamii, alitoa onyo kali, akisema vurugu
haziwezi kutoa suluhisho la kudumu bali husababisha athari zinazodumu kwa muda
mrefu, ikiwemo vifo na kuzorota kwa uchumi. Maoni haya yaliungwa mkono na
Thomas Kibwana, mchambuzi wa masuala ya kijamii, ambaye alieleza athari za moja
kwa moja za vurugu.
"Hatuwezi
kutatua changamoto zilizopo... kwa kutumia vurugu; badala yake, tunapaswa
kutatua changamoto tulizonazo kwa njia ya amani ili kuendelea mbele bila
kusababisha madhara ya kiuchumi nchini."
Kibwana
alitaja hasa uharibifu wa miundombinu ya usafiri, akisisitiza kuwa fedha za
maendeleo zinalazimika kuelekezwa kwenye ukarabati, hali inayosababisha raia
kupoteza muda wa uzalishaji.
Said
Miraji, mchambuzi wa siasa, alisisitiza kuwa amani lazima ianze kwa kila mmoja,
akisema haitoshi kuimba amani vinywani tu, bali tuishi amani mioyoni mwetu.
Alifafanua formula ya umoja: “Umoja unajengwa kwa imani, imani inajengwa kwa
usawa, na usawa unajengeka kwa kushirikiana.” Miraji alihimiza wazee kutoa
mfano bora kwa vijana.
Maoni
haya yanawiana na hisia za wananchi waliohojiwa.
Hollyess
Mbisse mkazi wa Dar es Salaam
alisisitiza kuwa amani ni "chanzo cha maendeleo" kinachotegemea
usalama na uhuru. Naye Deodatus Nyangwe
mkazi wa Dodoma alibainisha
jukumu la amani katika kukuza "uwekezaji nchini" na kuleta utulivu.
Aidha
Dorcas Kipangala (Dar es Salaam) alisisitiza kuwa amani ni msingi wa maisha na
muhimu kwa kufikishia sauti ya wananchi kwa serikali.
Ili
kudumisha amani na kuepusha vurugu zinazoharibu uchumi, Mchambuzi Miraji alitoa
wito kwa serikali: "Kuhakikisha inawawajibisha viongozi wasiokuwa
watendaji." Alieleza kuwa kutokuwajibika huunda changamoto za kijamii
zinazoweza kusababisha mifarakano.
Kwa
ujumla, wataalamu na wananchi wamekubaliana kwamba maendeleo ya taifa
yanategemea uwezo wa Tanzania kudumisha amani kwa matendo na kusuluhisha
changamoto zote kwa njia za amani, huku viongozi wakiwajibika kwa mahitaji ya
raia.

0 Maoni