RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi
amesema kuwa Serikali inalenga kuimarisha bajeti ya sekta ya elimu kutoka
shilingi Bilioni 864 hadi kufikia shilingi Trilioni 1.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira
bora ya ufundishaji, maslahi na posho za walimu pamoja na ujenzi wa miundombinu
ya elimu ili kuifanya Zanzibar kuwa na elimu bora.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 05
Disemba 2025 katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Jumuiya ya Walimu Wakuu
wa Skuli za Sekondari za Zanzibar (JUWASEZA), uliofanyika katika ukumbi wa
Skuli ya Fidel Castro sambamba na ufunguzi wa Dakhalia mpya ya wanafunzi wa
kike wa skuli hiyo iliyopo Mkoa wa Kusini Pemba.
Akizungumzia ujenzi wa Dakhalia, amesema ni mkakati
maalum wa Serikali wenye lengo la kuimarisha sekta ya elimu nchini. Ameeleza
kuwa Serikali itaendelea kujenga Dakhalia katika kila wilaya ili kufikia idadi
ya wanafunzi 10,000 wanaosoma katika skuli za Dakhalia ifikapo mwaka 2030.
Dkt. Mwinyi ametoa rai kwa walimu wakuu kuwa
wasimamizi madhubuti wa miundombinu ya elimu, ufaulu wa wanafunzi na rasilimali
za umma katika maeneo waliyopewa dhamana na kuahidi kutenga mafungu maalum ya
fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundimbinu ya elimu pale inapohitajika.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikisha walimu kuwa
Serikali ipo tayari kutatua changamoto zinazowakabili ili kuhakikisha
wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi ameahidi
kuyaangalia upya maslahi ya walimu wastaafu pamoja na watumishi wengine wa
sekta ya umma kwa lengo la kuimarisha maisha yao, ikiwemo upatikanaji wa nyumba
bora za kuishi, pensheni na posho.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Lela
Mohamed Mussa, amesema mageuzi makubwa yanayoendelea katika sekta ya elimu
yametokana na imani, maono na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Rais Dkt. Mwinyi
katika kuleta mageuzi na maendeleo ya sekta hiyo.
Amebainisha kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa katika
sekta hiyo, hususan katika miundombinu ya elimu, umeongeza ari ya walimu
kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi.
Akitoa taarifa ya kitaalamu ya ujenzi wa Dakhalia ya
wanafunzi wa kike, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis
Abdallah Said, amesema ujenzi huo umegharimu shilingi Bilioni 1.5 na una uwezo
wa kuchukua wanafunzi 288 kwa wastani wa wanafunzi 28 kwa kila darasa. Aidha,
amesema Wizara ya Elimu inakusudia kujenga Dakhalia nyingine 16 Unguja na Pemba
katika mwaka wa fedha wa 2025–2026.
Mradi wa Dakhalia ya wanafunzi wa kike wa Skuli ya
Fidel Castro unakuwa mradi wa kwanza kufunguliwa na Rais Dkt. Mwinyi kisiwani
Pemba tangu alipochaguliwa tena kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi kuiongoza tena Zanzibar kwa kipindi cha pili cha Awamu ya Nane.


0 Maoni