Wiki chache baada ya ghasia na vurugu zilizofuatana na uchaguzi, Watanzania kutoka maeneo mbalimbali wamejitokeza kwa umoja kutoa tamko la dhati la kuahidi kuilinda amani, wakibainisha kuwa matukio hayo yaliwaacha na somo la maumivu.
Kauli
za wananchi zilizosambaa mitandaoni zinaonyesha mwafaka wa kitaifa unaopita
mipaka ya kijiografia: "Kutoka Arusha hadi Mbeya, kutoka Mwanza hadi
Songwe, Watanzania wanasema kwa sauti moja: Amani ndiyo njia, na sisi ndio
walinzi wake."
Miongoni
mwa walioeleza athari za vurugu hizo ni Bi. Witness Rabson Nkini, mkazi wa
Mvuti, Dar es Salaam, ambaye biashara yake iliathirika moja kwa moja. Witness
alieleza jinsi uchafuzi wa amani ulivyosimamisha maisha yao na kuwalazimu
kutumia fedha nyingi katika kununua vyakula.
"Kipindi
cha uchaguzi kulikuwa na mtafaruku, kulikuwa na maandamano, ikatupelekea
kufunga ofisi zetu. Kama mimi hapa nafanya saluni, tumekosa fedha. Tukikosa
fedha tukalamzika kutumia fedha nyingi kununua vyakula," alieleza Witness.
Alisisitiza
kuwa matukio hayo yamepelekea kupungua kwa amani si tu kwa watu wazima, bali
pia kwa watoto wao, akitoa wito: "Tunaomba tuwe na amani na upendo.
Wengine tunawatoto wanakosa amani."
Ushuhuda
wa Witness na wengine unaakisi hali halisi ya Watanzania wengi ambao sasa
wanaeleza kwamba, "Tumepitia maumivu, tumejifunza somo. Leo tunachagua
amani, kwa ajili ya familia zetu, kazi zetu na mustakabali wa Tanzania."
Kauli
hizi zimeungwa mkono na jumbe mbalimbali zinazosisitiza:
"Watanzania
hili Ni somo tumejifunza tuilinde amani. Amani ni tunu yetu."
"Uchafuzi
wa amani hauna faida. Tuungane kuilinda nchi yetu."
"Maandamano
ni biashara, wachache inawalipa na kuwanufaisha zaidi huku wengi tukiumia kwa
kupoteza kazi, biashara zetu na madhara mengine mengi."
Wananchi
wengi wameahidi kuendelea kuienzi amani kama msingi wa maendeleo, huku
wakihimiza: "Kesho bora ya Tanzania itajengwa kwa kuendelea kuenzi amani,
kuvumiliana na kushirikiana."
Katika
kuimarisha azma ya kudumu ya amani, kuna wito wa dhati wa kuwaepuka wale wote
wanaoweza kuvuruga utulivu wa taifa. Ujumbe ulioenea unasema: "Tusitoe
nafasi kwa watovu wa amani nchini mwetu kuja kuvuruga amani, upendo na
mshikamano tulionao."
Wengi
wamekubaliana kuwa "Amani si tukio, ni maamuzi ya kila siku. Tuanze leo,
kwa maneno yetu, matendo yetu, na mioyo yetu."

0 Maoni