Serikali
imesema itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji
kwa Jamii (CSR) inayotekelezwa na kampuni za uchimbaji madini nchini, ili
kuhakikisha wananchi wanaoishi jirani na migodi wananufaika moja kwa moja na
shughuli za uchimbaji madini.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, Mayigi Makolobela, alisema hayo hivi karibuni alipokagua utekelezaji wa miradi ya CSR inayofanywa na kampuni za uchimbaji madini katika mkoa huo, akibainisha kuwa miradi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na miundombinu ya umeme.
“Serikali
inatambua mchango mkubwa wa sekta ya madini katika kukuza uchumi wa nchi na
kuboresha maisha ya wananchi. Ndiyo maana tunasisitiza kampuni zote za
uchimbaji, zikiwemo zinazomilikiwa na wachimbaji wadogo, kutekeleza wajibu wao
wa kijamii kupitia miradi ya CSR ili jamii inayoishi jirani na migodi inufaike
moja kwa moja na rasilimali hizo,” alisema Makolobela.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya EMJ Mining iliyopo eneo la Dutwa mkoani Simiyu,
Masanga Silanga, alisema kampuni hiyo inajihusisha na uchimbaji wa dhahabu kwa
ushirikiano na wawekezaji kutoka China, jambo lililoongeza ufanisi na
teknolojia katika shughuli zao za uchimbaji.
Alisema
kampuni hiyo huzalisha wastani wa kilo 10 za dhahabu kwa mwezi endapo kuna
upatikanaji mzuri wa mwamba wenye madini (mbale), ingawa wakati mwingine
hukumbwa na changamoto ya upatikanaji wa mwamba kutokana na baadhi ya maeneo
kuwa na mishororo midogo ya dhahabu (narrow vein).
Silanga
alibainisha kuwa kampuni yake imetekeleza miradi kadhaa ya CSR ikiwemo kutoa
madawati 50 na matofali 2,000 kwa Shule ya Msingi Dutwa, mashine za kuchapisha
(printer) na nakala (photocopy) kwa taasisi za elimu, pamoja na mchango wa
matofali 2,000 kwa Hospitali ya Nguno.
“Tayari
tumewekeza zaidi ya Dola 50,000 katika miradi ya CSR, ikiwemo mradi wa kuvuta
umeme kutoka Dutwa hadi vijiji vya jirani ambavyo awali havikuwa na huduma ya
umeme,” alisema Silanga.
Naye Meneja
wa Mgodi huo, Noah Wang, alisema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kwa sasa
ni upungufu wa mwamba wenye madini (mbale), hali inayosababisha baadhi ya
mitambo kusimama na kupunguza uzalishaji.
“Mitambo
yetu ina uwezo wa kuchakata hadi tani 500 za mwamba kwa siku, lakini kwa sasa
hatupati kiwango hicho, jambo linalolazimisha baadhi ya mitambo kuzimwa mara
kwa mara. Kwa sasa shaft moja pekee ndiyo inaendelea na kazi, hivyo uzalishaji
umeshuka kwa kiasi kikubwa,” alisema Wang.
Aliongeza
kuwa kampuni hiyo imeajiri jumla ya wafanyakazi 48, wakiwemo 30 wazawa na 18
raia wa China, wanaofanya kazi kwa mfumo wa
kupokezana (shift system).




0 Maoni