Athari
za uchochezi na vurugu za kisiasa zimeonekana wazi nchini, huku wananchi
wakijifunza somo gumu kuhusu thamani ya amani. Sauti za maumivu na majuto sasa
zimegeuka kuwa wito wa umoja, huku vijana wakihimizana kujiepusha na habari za
uchochezi na kuelekeza nguvu zao kwenye
shughuli za uzalishaji.
Bi.
Faudhia Ramadhani, mkazi wa Chanika, ni miongoni mwa wananchi waliohisi maumivu
ya machafuko hayo, akitoa ushahidi wa athari hizo.
“Kilichotokea
sitamani tena kijirudie. Tunapenda tuwe na amani, hatutaki tena itokee kama
ilivyotokea. Tumeona kilichotokea, tumehisi maumivu, na sasa tumejifunza,”
ameeleza Faudhia.
Kauli
yake inaunga mkono hisia za Watanzania wengi, ambao wamekiri kwamba uwepo wa
vurugu kipindi cha uchaguzi ulipelekea wananchi kuwa na hofu, kukimbia biashara
zao na makazi yao, na kupoteza baadhi ya mali na kukosa mahitaji muhimu ya kila
siku kwa siku kadhaa.
“Vurugu
zimewaumiza wananchi,” alisema mmoja wa wachangiaji, akisisitiza kuwa amani ni
maendeleo.
Faudhia
Ramadhani ametoa wito mzito kwa vijana wenzake, akihimiza kipaumbele kipya cha
maisha: kazi badala ya machafuko.
“Nawashauri
vijana wenzangu tusijihusishe na machafuko yoyote yale. Wito wangu ni tufanye
kazi tuachane na habari za uchochezi,” amesisitiza Faudhia.
Ujumbe
huu umepokewa vyema na vijana wengine, ambao wamekiri kuwa ni jukumu lao
kulinda amani. Kauli mbiu mpya imejitokeza: “Tufanye Kazi, Si Kelele; Tanzania
Inahitaji Maendeleo, Si Maandamano.”
Wananchi
mitandaoni na katika vijiwe mbalimbali wanakumbushana kuwa, ingawa vurugu
ilichoma mali, haikuweza kuchoma roho ya Tanzania. “Leo tunasimama tena, tukiwa
wamoja, tukiitazama amani kama mwanga wa kesho yetu,” walisema.
Vijana
wanakumbushwa kuwa amani hii inatakiwa kulindwa kwa wivu mkubwa na kwamba wao
ndio dhamana ya taifa hili. Wanahimizana kuendelea kuwa mstari wa mbele
kuhubiri amani kupitia maridhiano.
Kama
Faudhia anavyosisitiza, vijana wajiepushe na vyanzo vyote vya habari
vinavyolenga kuchochea chuki na kugawanya taifa, ili kulinda msingi wa amani
ambao ni muhimu kwa maisha na maendeleo yao binafsi na ya
nchi kwa ujumla.

0 Maoni