Tanzania ni nchi changa, yenye
nguvu kubwa ya vijana. Wao ndio uti wa mgongo wa taifa, nguvu kazi ya
uzalishaji, na chemchemi ya ubunifu. Lakini nguvu hii kubwa inahitaji mwelekeo
sahihi, hekima, na maadili ya kizalendo, hasa katika zama hizi za propaganda za
kidijitali.
Katika enzi hizi za habari za
kasi, vijana wanatumia mitandao ya kijamii kama chombo cha mawasiliano, lakini
mitandao hii pia imekuwa uwanja wa chuki, upotoshaji, na ajenda za siri.
Bw. Lugete Mussa, mchambuzi wa
siasa na diplomasia, anasema kuwa baadhi ya mataifa yenye maslahi ya kiuchumi
na kisiasa hutumia habari potofu kuvuruga umoja wa Watanzania.
“Vijana lazima waamke. Wasiwe
sehemu ya ajenda za watu wanaotaka kuumiza taifa lao kwa jina la demokrasia au
haki,” alisema Bw. Lugete.
Kauli yake ni wito wa kizalendo
kwa vijana kutambua kuwa taifa linajengwa kwa umoja na maelewano, si kwa
kugawanyika na hasira.
Wataalamu wa jamii wanaeleza kuwa
vijana wengi wanasukumwa na hasira, wivu, au tamaa ya mafanikio ya haraka, hali
inayowafanya waamini kila kitu wanachokiona mtandaoni. Huu ni mtego wa fikra
unaotengenezwa makusudi na wapotoshaji ili kuvunja imani ya vijana kwa nchi
yao.
Kijana kutoka Dodoma, Bw. Hussein
Thomas Mwanga, anaakisi mwamko huu mpya. “Mpaka leo siamini kile kilichotokea
Oktoba 29. Nilijifunza kuwa amani haihitaji kelele, inahitaji fikra sahihi. Ni jukumu
letu vijana kuitetea amani.”
Maneno yake yanatoa nuru kwamba
amani haiwezi kudumu bila haki, lakini haki haiwezi kupatikana kwa ghasia.
Tunapodai haki, ni lazima tuikumbuke amani kama chombo cha mazungumzo.
Kizazi cha sasa kinapaswa kuelewa
kwamba mitandao si mwalimu wa ukweli. Ni kioo kinachoonyesha taswira kulingana
na macho ya anayeitazama. Vijana wanapaswa kutumia muda mwingi kujifunza,
kuanzisha miradi, na kutafuta maarifa badala ya kushiriki mijadala ya chuki.
Mchambuzi mmoja wa ajira alieleza
ukweli mchungu wa vurugu: “Kila kituo cha mafuta kilichochomwa hakikuwa jengo
tu lililoungua, bali ni ndoto, ajira, na maisha ya vijana halisi
yaliyoteketezwa.”
Wale wanaochochea vurugu
mtandaoni mara nyingi hawapo katika uhalisia wa maumivu yanayofuata. Wanatuma
ujumbe kutoka umbali salama, lakini vijana wanaowaamini wanajikuta wakipoteza
maisha, kazi, na heshima zao.
Uzalendo wa kweli haupimwi kwa
maneno makali ya mitandaoni, bali kwa matendo. Vijana wazalendo ni wale
wanaoandika ujumbe wa matumaini, wanaolinda heshima ya nchi yao, na wanaochagua
utulivu badala ya fujo.
Bw. Lugete aliongeza kuwa kila
kijana ana jukumu la kuilinda taswira ya Tanzania, maana heshima ya taifa
haijengwi na viongozi pekee, bali na wananchi wenye uelewa na nidhamu ya fikra.

0 Maoni