
Askofu Israel Maasa, Katibu wa
Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), amesisitiza umuhimu wa
kuitekeleza kwa vitendo falsafa ya 4R iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Maridhiano
(Reconciliation),Ustahimilivu (Resilience),Mageuzi (Reforms) na Kujenga Upya
(Rebuilding).
Askofu Maasa ameeleza kuwa
falsafa hii ni tiba muafaka kwa majeraha ya kisiasa na kijamii yaliyotokana na
uchaguzi. “Si lazima tukubaliane katika kila jambo, lakini tunaweza kukubaliana
katika kutokukubaliana kwa amani. Tunahitaji diplomasia zaidi,” aliongeza Askofu
Maasa.
Kwa waamini wa dini tofauti,
kauli hii imekuwa mwanga wa matumaini. Hekima ya kuketi meza moja,
kusikilizana, na kusamehe inajenga imani ya kitaifa.
Viongozi wa dini wanaamini kwamba
maombi na msamaha ni dawa sahihi ya kuponya majeraha ya mioyo ambayo siasa peke
yake haiwezi kuyaponya.
Akisisitiza umuhimu wa amani,
mwanasiasa mkongwe kutoka mkoani Arusha, Modesti Meikoki, alieleza kuwa hakuna
sababu ya kuruhusu maandamano au hasira za kisiasa kugawanya taifa. Alisema,
“Matukio yaliyotokea yameleta taharuki kwa wapenda amani duniani. Tuna wajibu
wa kurejea katika maadili ya Kikristo na Kiislamu yanayohimiza amani,
mshikamano, na utii kwa sheria.”
Viongozi wa dini wametoa wito kwa
wananchi kurejelea utu na busara katika maamuzi yao ya kila siku. Wamehimiza
kuepuka chuki, kulinda lugha yetu mtandaoni, na kuchagua mazungumzo badala ya
mabishano. Katika maombi ya kitaifa yaliyofanyika Dodoma mwezi Novemba 2025,
kiongozi mmoja wa dini aliwakumbusha waumini kwamba amani haiwezi kujengwa kwa
matusi, bali kwa huruma na heshima.
Kama viongozi wa dini
wanavyokumbusha, tuendelee kuomba na kufanya kazi kwa amani. Tuendelee kujenga
madaraja ya maelewano badala ya kuta za mabishano. Kwa upendo, kwa huruma, na
kwa imani, Tanzania itaendelea kusimama kama mfano wa amani barani Afrika.
0 Maoni