WACHIMBAJI
Wadogo wa Madini wa Mkoa wa Simiyu wameiomba Serikali pamoja na taasisi za
kifedha kuwaunga mkono kwa kuwapatia umeme wa kudumu na mikopo yenye masharti
nafuu, wakisema changamoto hizo zimekuwa kikwazo kikubwa katika kuongeza
uzalishaji wa madini, hususan dhahabu.
Mmoja wa
wachimbaji wanawake kupitia Chama cha Wachimba Madini Wanawake Tanzania
(TAWOMA) mkoani humo, Anisia Japhet, amesema wamekuwa wakitumia gharama kubwa
kuendesha mitambo kutokana na kutegemea nishati ya dizeli.
“Tunatumia
dizeli ambayo ni ghali. Lita 80 zinamalizika ndani ya saa 24. Tungepata umeme
wa kudumu, tungepunguza gharama na kuongeza tija,” amesema Anisia.
Ameongeza
kuwa uchimbaji si kazi ya wanaume pekee bali ni fursa yenye manufaa makubwa kwa
wanawake wanaojituma.
“Nikiwa
mwanamke, nimefanikiwa kusomesha watoto na kuendesha maisha yangu kupitia
uchimbaji. Kila mwezi tunapata wastani wa viroba 100 vya mawe, na kila kiroba
kinaweza kutoa gramu moja au zaidi za dhahabu,” ameongeza.
Kwa upande
wake, Meneja wa Mgodi wa TAWOMA, Paul Ntalima, amesema wanamiliki maduara 24 ya
uzalishaji, lakini ni maduara 14 pekee yanayoendelea na kazi kutokana na
gharama kubwa za uendeshaji.
“Wachimbaji
wadogo wana uwezo wa kuongeza tija mara mbili zaidi endapo watapatiwa mikopo
yenye riba nafuu. Tunatengeneza ajira kwa vijana na wanawake zaidi ya 400.
Sekta hii si tu inaleta kipato, bali pia inaimarisha maisha ya wananchi.
Tukipata umeme wa gridi, uzalishaji utaongezeka mara mbili hadi tatu,” amesema
Ntalima.
Naye Mussa
Kazidijshi, Mtendaji wa Mgodi wa Ludovic Mlalo & Partners, amesema mgodi
wao unaajiri zaidi ya wafanyakazi 200 na umeendelea kurejesha kwa jamii kupitia
miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara.
“Jamii
inanufaika hasa wakati wa mvua ambapo barabara huboreshwa na milipuko ya
magonjwa hupungua. Tukipatiwa mikopo ya riba nafuu na nishati ya kudumu ya
umeme, uzalishaji wetu utaongezeka mara tatu,” amesema Kazidijshi.
Akizungumzia
changamoto hizo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, Mayigi Makolobela,
amesema Serikali kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na TANESCO inaendelea
na mazungumzo kuhakikisha maeneo yote ya wachimbaji wadogo mkoani humo
yanapatiwa umeme wa kudumu.
“TANESCO wameahidi kufikisha umeme katika maeneo yote ya wachimbaji wadogo mkoani Simiyu ili kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama za uendeshaji,” amesema Makolobela.
Ameongeza
kuwa Serikali inaendelea na mpango wa kufanya tafiti zaidi katika maeneo ya
madini ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya uchimbaji wenye tija.
“Wito wangu
kwa taasisi za kifedha ni kuangalia upya namna ya kuwakopesha wachimbaji
wadogo, kwa kuwa wana bidhaa halisi, masoko yapo, na taarifa zao za kifedha
zinajulikana. Wana uwezo wa kurejesha mikopo,” amesisitiza Makolobela.
Amebainisha
kuwa kwa sasa Mkoa wa Simiyu una vituo vitano vya ununuzi wa madini na soko kuu
moja lililopo Bariadi Mjini, ambako shughuli kubwa za biashara ya madini
hufanyika.
Makolobela
pia amewapongeza wachimbaji kwa kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii
kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), akitaja mfano wa vikundi vya
TAWOMA na EMJ vilivyotoa zaidi ya madawati 90 kwa Shule ya Majengo kama sehemu
ya kurudisha kwa jamii.



0 Maoni