Mkoa wa Mbeya umerejea katika
utulivu kamili huku shughuli za kibiashara na kijamii zikichukua kasi, kufuatia
siku chache za vurugu za kisiasa zilizogharimu maisha na mali. Kurejea huku kwa
hali ya kawaida kumeambatana na sauti za wananchi zilizojawa majuto na
msisitizo mkubwa wa thamani ya amani na utulivu.
Wananchi wa Mbeya, ambao wengi
wao hutegemea mapato ya kila siku, wameeleza jinsi vurugu hizo zilivyowaathiri
moja kwa moja.
Tuli Kyando, mfanyabiashara mkazi
wa Uyole, amesema vurugu zimeacha vilio na hasara kubwa kwa wafanyabiashara.
“Siku tatu tulizokaa nyumbani zimenigharimu sana kibiashara. Maisha ya
Mtanzania ni kutoka na kutafuta chakula cha siku hiyo,” ameeleza Kyando.
Amesisitiza kuwa vitendo
walivyofanya vijana vilikuwa si vizuri, kwani vimeharibu uwekezaji ambao ni
ajira za watu kwa kuchoma moto mali zilizokuwepo. Amewataka vijana kuacha
kutumia hasira na badala yake waone namna bora ya kufanya mambo, ikiwemo kukaa
chini na kuzungumza.
Naye Nico Lawio Njowela, mkazi
mwingine wa Mbeya, amesisitiza umuhimu wa kufuata sheria. “Kwa sisi vijana,
tunapokuwa na changamoto za maisha, ni vizuri tukafanya mambo kwa kufuata
viongozi na sheria ili kupata suluhisho, kuliko kuchukua sheria mkononi.
Watanzania ambao tuna hali ya chini tuliteseka sana kwenye hii vurugu,” amesema
Njowela.
Kufuatia hasara hiyo, jumbe za
wananchi mitandaoni zimejikita katika kukataa uchochezi na kuwataka Watanzania
waungane kulinda nchi yao. Wengi wamehoji mantiki ya vurugu wakisema
inafaidisha wachache tu.
“Maandamano ni biashara, wachache
inawalipa na kuwanufaisha zaidi huku wengi tukiumia kwa kupoteza kazi, biashara
zetu na madhara mengine mengi,” alieleza mmoja wa wajasiriamali.
Wananchi wamesisitiza kuwa
tofauti za kisiasa hazipaswi kamwe kuharibu amani. Wamekariri msemo kuwa,
“Amani huleta fursa kwa vijana na maendeleo; tuzidi kuwa imara katika kulinda
Amani ya nchi yetu.”
Katika kuendeleza umoja, ujumbe
mkuu wa wananchi ni wito wa kuaminiana na kujitenga na wapotoshaji.
“Uchochezi huu umeleta madhara
makubwa sana, tusikubali kutumika kisiasa na wanaharakati,” ulisema ujumbe
mmoja.
“Tuipende nchi yetu kwa kudumisha
amani na upendo,” uliongeza mwingine.
Kama somo la vurugu hizo,
wananchi wanakumbushana: “Siku moja ya vurugu ilitufundisha thamani ya miaka
yote ya amani. Tuliona hasara, tukasikia vilio, lakini sasa tumejifunza. Leo
tunasema: tusirudie kosa hili, tuishi kwa upendo, tujenge kwa amani.”

0 Maoni