WAZIRI MKUU,
Dkt. Mwigulu Nchemba leo Novemba 15, 2025 amefanya ziara ya kushtukiza katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuziagiza hospitali zote nchini
zihakikishe wajawazito wanapofika hospitali wahudumiwe kwa haraka ili kuokoa
maisha ya mama na mtoto.
Pia, Waziri
Mkuu ameiagiza Wizaya ya Afya, Bohari ya Dawa (MSD) na Hospitali zote nchini
ziweke vipaumbele vya kuwa na dawa kulingana na mahitaji ya eneo husika. “
Haipendezi mwananchi kufika hospitali na kupatiwa vipimo vyote kisha anaambiwa
dawa akanunue kwingine, kama duka binafsi linaweza kupata dawa hizo,
inawezekanaje hospitali za serikali hapati? Naagiza Hospitali zote ziwe na
dawa.”
Ametoa
maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi nje ya hospitali hiyo baada ya
kutembelea wananchi waliofika hospitalini hapo kupata huduma mbalimbali za
kitabibu ambapo amesisitiza wananchi waendelee kuhudumiwa vizuri kwa kuwa
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya
kuboresha huduma za afya nchini vikiwemo vifaa tiba na dawa.
Kadhalika
Mheshimiwa Waziri Mkuu ameziagiza hospitali zote nchini zihakikishe zinakuwa na
vifaa vya usafi binafsi vya dharura vikiwemo ndoo na beseni katika wodi za
wazazi ili viwasaidie akinamama wasiokuwa na vifaa hivyo. “Ujauzito sio suala
la dharura vifaa kama ndoo tunapaswa kuwa navyo katika hospitali zetu za
serikali.”
Dkt. Mwigulu
ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kazi kubwa anayoifanya katika uboreshaji wa huduma za afya nchini. Waziri Mkuu
akiwa hospitalini hapo, wananchi
walimueleza kuwa wanahudumiwa vizuri na kwa uangalizi wa karibu.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza hospitali zote nchini zizingatie maelekezo ya
kutumia mifumo sahihi ya malipo katika taratibu za kutoa huduma ili kuwezesha
Serikali kuendelea kuhudumia wananchi.
Dkt. Mwigulu
ametoa agizo hilo kufuatia kuwepo kwa hospitali ambazo baadhi ya huduma
wanapokea malipo kwa njia ya mtandao na nyingine malipo yanapokelewa malipo kwa
njia zisizo rasmi.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti wagonjwa na wananchi wanaoguza ndugu zao wamempongeza
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa
huduma bora za afya.
“Tunamshukuru
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa tunapatiwa huduma nzuri kama
tupo hospitali za private (binafsi).”
Kauli hiyo imetolewa na Dinna Enock, mkazi wa Makulu jijini Dodoma
ambaye amelazwa katika wodi ya wazazi.



0 Maoni