Mbunge wa Kilosa, Profesa
Palamagamba Kabudi, amesema hotuba aliyoitoa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13 imewapa Watanzania mwanga mpya na kuongeza
imani juu ya safari ya maendeleo kwa miaka mitano ijayo.
Akichambua hotuba hiyo, Prof.
Kabudi alibainisha kuwa uthabiti wa Rais Samia na namna anavyowajali wananchi
ndivyo vimeleta faraja kubwa nchini.
Profesa Kabudi alinukuu kitabu
cha hayati Shaban Robert cha ‘Kusadikika’ akisema: "katika nyakati ngumu
huzaa viongozi thabiti." Alieleza kuwa katika kipindi hiki cha changamoto,
Rais Samia ameonesha ujasiri na uthabiti wake wa kipekee.
'Uthabiti huu sio tu wa
kuomboleza na kutambua msukosuko uliokuwepo nchini, bali pia ameonesha
matumaini na nyenzo za kutimiza matumaini hayo,' alisema Prof. Kabudi.
Aliongeza kuwa ahadi za Rais
Samia za kuanzisha Madirisha ya Uwekezaji na kutenga shilingi bilioni 200 kwa
ajili ya mitaji kwa vijana zitabadili maisha yao.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi,
hotuba ya Rais Samia ilikuwa ni mfariji mkubwa kwa Taifa hasa pale
alipozungumzia kaulimbiu ya Serikali ya 'Kazi na Utu'.
Rais Samia alisema anatamani
Awamu yake ya Sita ikimalizika, ikumbukwe si kwa sababu ya ujenzi wa
miundombinu mikubwa pekee, bali kwa sababu utu wa Mtanzania uliendelezwa na
kupewa thamani kubwa.
"Msisitizo aliouweka Rais
katika kushughulikia changamoto za watu wa kawaida umeleta faraja. Alizungumzia
kwa ujasiri kuhusu uponyaji wa Taifa, akitangaza Tume ya Uchunguzi na kutoa
msamaha kwa vijana wa mkumbo. Hii inaonyesha kiongozi ambaye anajali utu zaidi
ya siasa," alimalizia Prof. Kabudi.
Maneno haya ya Mbunge huyo
yanathibitisha kuwa, hotuba ya Dkt. Samia ilikuwa na lengo la kuunganisha
Taifa, kulipa faraja, na kuliweka kwenye njia thabiti ya maendeleo yenye utu.

0 Maoni