Madhara ya vurugu hayako tu kwenye uharibifu wa mali
na uchumi, bali pia kwenye afya ya akili ya wananchi. Watu wengi walibaki na
hofu na kiwewe (trauma) kisaikolojia hata baada ya hali kutengemaa, hofu
iliyosababisha kutokuwa na ujasiri wa kurudi kwenye majukumu yao.
Siraji Ali Likwati anathibitisha hofu hii:
"Mimi mpaka leo hii nakuambia ndio naingia kazini kwa sababu pamoja na
kuambiwa kuko shwari nilikuwa sijiamini. Leo ndio nakuja kuangalia tu mambo
yanakwenda vizuri." Hofu hii ilisababisha hasara ya siku za kazi.
Daktari wa Afya ya Akili anasisitiza: "Wakati
wa vurugu, watu hupatwa na Acute Stress Disorder. Tunahitaji haraka programu za
ushauri nasaha za jamii, hasa katika maeneo yaliyoathirika. Kuponya akili ni
muhimu kama kuponya majeraha ya mwili."
Kiongozi mmoja wa Dini, Paul Koba kutoka dhehebu
moja anaongeza: "Katika kitabu cha Kibiblia, tunafundishwa kuwa na 'amani
ipitayo akili yote' (Filipi 4:7). Kusamehe na kusahau ni dawa kubwa ya kuponya
kiwewe na kurudisha amani ya moyo na utulivu wa kufanya kazi kwa bidii."

0 Maoni