Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito mzito kwa vijana wa taifa
kuilinda amani ya nchi na kukataa kwa nguvu zote kushawishiwa kuingia kwenye
vitendo vinavyohatarisha utulivu wa Tanzania.
Akihutubia Bunge la 13 jijini
Dodoma , Ijumaa Novemba 14, 2025, Dkt. Samia alitoa ujumbe wa upatanishi na
msamaha, huku akisisitiza kuwa vijana ndio walinzi na wajenzi wa taifa, hivyo
hawapaswi kutumia mikono yao kuivunja nchi iliyojengwa kwa amani, jasho na
uvumilivu.
“Msikubali kukata tawi la mti
mnaoukalia. Msikubali kushawishiwa kuichoma Tanzania. Nyinyi ndio walinzi wa
Taifa hili, wajenzi wa kesho yake, kamwe msije kuwa wabomoaji,” alisema Rais
Samia, akipokea shangwe kutoka Bungeni.
Katika wito huo huo wa kujenga
umoja na matumaini, Dkt. Samia alitangaza hatua kubwa ya msamaha, akielekeza
Ofisi ya Mashtaka (DPP) kuwafutia makosa vijana wote waliojiingiza katika
vurugu za Oktoba 29, 2025, kwa kufuata mkumbo na ushabiki bila dhamira ya
kufanya uhalifu.
“Nikiwa mama na mlezi wa Taifa
hili, ninaviomba vyombo vya sheria na hasa Mkurugenzi wa Mashtaka kuangalia
kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana wetu. Kwa wale ambao walijiingiza kwa
mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu, wasamehewe,” alisisitiza kiongozi
huyo.
Alifafanua kuwa ushahidi wa video
unaonyesha wazi kuwa baadhi ya vijana hawakujua uzito wa walichokuwa wakifanya.
Akitoa rejea ya kiroho, Rais Samia alikumbusha, “Natoa msamaha huu kwa sababu
hata maneno ya Mwenyezi Mungu katika Kitabu cha Luka 23:34 yanasema ‘Baba
uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.’”
Rais Samia alihitimisha kwa
kuwakumbusha Watanzania kutanguliza maelewano, ushirikishwaji, na umoja katika
safari ya kuelekea miaka mitano ijayo ya Serikali ya Awamu ya Sita, akisisitiza
kuwa taifa linahitaji vijana wenye uelewa, walio tayari kujenga
badala ya kubomoa.

0 Maoni