RAIS wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea
kuwasisitiza Watanzania waendelee kuliombea Taifa ili amani, upendo,
ustahimilivu na mshikamano viendelee kudumu nchini.
Kauli hiyo
imetolewa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba leo (Jumapili, Novemba 16, 2025)
alipowasilisha salamu za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa waumini
na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa
Kisasa, Mkoa wa Dodoma.
“Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawasalimu sana. Yuko pamoja nanyi, na rai yake
kwa Watanzania wote ni kuendeleza maombi kwa Taifa letu kuwa watulivu na
kuiombea amani iendelee kudumu.”
Aidha,
Waziri Mkuu amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha amani ya nchi
inaendelea kulindwa na kuenziwa, kwa sababu pasipo amani, Taifa halitoweza
kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuendesha ibada na shughuli nyingine za
kijamii.
“Pasipo
amani hatuwezi kutekeleza majukumu mengine yoyote, pasipo amani hatuwezi
kuendesha ibada. Hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuiombea nchi yetu. Pakiwa
na amani tunaweza kutekeleza yale yaliyo katika matarajio yetu, tunaweza hata
kutatua yale tunayoyaona kuwa ni magumu.”
Ibada hiyo
imeongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma, Dkt. Christian Ndossa ambaye
ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Watanzania waishi kwa kumtanguliza Mungu mbele
na wawe na matumaini kwake na wajiepushe na maovu.
Mheshimiwa Dkt.
Mwigulu ameambatana na Mwenza wake, Mama Neema Mwigulu Nchemba, katika ibada
hiyo.
Viongozi
wengine waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Naibu Spika wa Bunge, Daniel
Sillo, Mbunge wa Kilolo, Ritha Kabati, Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya,
Mbunge wa Viti Maalumu, Balozi Dkt. Pindi Chana, Mbunge wa Itigi, Yohana Msita
na Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba na mkewe Mama Neema Mwigulu Nchemba wakishiriki katika Ibada ya Jumapili kwenye Usharika wa KKKT Kisasa jijini Dodoma, Novemba 16, 2025. Kulia ni Naibu Spika wa Bunge Daniel Sillo.



0 Maoni