MKOA wa
Kimadini wa Mahenge umeanza kwa kasi katika ukusanyaji wa mapato ya madini kwa
mwaka wa fedha 2025/2026, baada ya kukusanya shilingi milioni 270 ikiwa ni
asilimia 62 ya lengo la shilingi milioni 433 la kipindi cha kuanzia mwezi Julai
hadi Oktoba, 2025. Lengo la mwaka lililowekwa ni shilingi bilioni 1.3.
Akizungumza
na waandishi wa habari, hivi karibuni Afisa Madini Mkazi wa Mahenge (RMO),
Jonas Mwano, alisema mafanikio hayo yametokana na ongezeko la uzalishaji wa
madini ya vito pamoja na kuimarika kwa mifumo ya usimamizi na udhibiti wa
rasilimali hizo.
Mwano
alibainisha kuwa Mahenge, inayojumuisha wilaya za Ulanga, Kilombero na Malinyi,
imeendelea kuwa kitovu cha uzalishaji wa madini ya vito, madini ya viwandani
kama graphite, pamoja na madini ya ujenzi ikiwamo kokoto, mchanga na mawe.
Alisema
licha ya eneo hilo kutegemea zaidi uzalishaji wa madini ya vito, miradi mikubwa
ya kimkakati inayotarajiwa kuanza utekelezaji itachochea kwa kiwango kikubwa
ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.
“Miradi hiyo
inajumuisha kampuni za Faru Graphite na Duma ambazo tayari zimepata leseni na
zinajiandaa kuanza uzalishaji,” alisema.
Kwa mujibu
wa Mwano, miradi hiyo itachangia kuboresha miundombinu ya Mahenge ikiwamo
upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya migodi na matumizi ya majumbani,
pamoja na ujenzi wa barabara za lami.
“Barabara
kutoka Ifakara hadi Ulanga imekuwa changamoto kwa muda mrefu. Ili makontena ya
Kinywe yasafirishwe kwa usalama, lazima kuwe na barabara ya uhakika. Tuna
matumaini uwekezaji huu utafungua ukurasa mpya,” alisisitiza.
Aidha,
alisema kampuni hizo zinatarajiwa kutoa ajira kwa wananchi wa eneo hilo, ambapo
Faru Graphite itaanza kwa kuajiri watu 500, huku Duma ikitarajia kutoa ajira
300.
Kwa upande
wao, wachimbaji wadogo wameiomba Serikali kuangalia namna ya kurahisisha
upatikanaji wa madini katika masoko ya ndani.
Khalid
Njechere, mnunuzi wa madini ya vito, alisema baadhi ya wawekezaji wakubwa
wanauza madini nje ya nchi kwa kibali maalum, hali inayowaacha wachimbaji
wadogo bila malighafi ya kutosha.
“Tunaomba
Serikali ifanye mazungumzo na wawekezaji wakubwa ili angalau sehemu ya madini
yao ibaki hapa nchini. Sokoni tunapata changamoto kubwa kupata madini,”
alisema.
Kwa upande
wake, Meneja Msaidizi wa Kampuni ya RGI, Shafii Daome, alisema kampuni hiyo
inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya spinel imeajiri Watanzania 64 na
wageni sita, huku ikiendelea kutekeleza miradi ya kijamii ikiwamo ujenzi wa
ofisi za kata na uchongaji wa barabara ya kilomita saba ambayo imekuwa ikileta
changamoto wakati wa mvua.
Daome
alisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali kuboresha mazingira ya
kiuchumi na kijamii kwa wananchi wanaoishi jirani na
maeneo ya machimbo.




0 Maoni