Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, ametoa wito wa kutekelezwa kwa kasi kubwa, maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanayolenga kurejesha haraka utoaji wa huduma za umma kwa wakazi wa Ilala kufuatia vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi.
Akizungumza na watendaji wa
wilaya hiyo, DC Mpogolo alisisitiza umuhimu wa kurejesha hali ya kawaida,
kuanzia katika miundombinu ya ofisi za umma.
"Tunapaswa kutekeleza
maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kasi kubwa ya kuhakikisha
tunarudisha utoaji wa huduma kwa Wana Ilala. Kwa pamoja tumedhamiria kujenga
Ofisi zetu na tuweze kuwahudumia watu," alisema Mhe. Mpogolo.
DC Mpogolo alipongeza vikosi vya
ulinzi na usalama kwa kazi yao ya kudhibiti hali ya usalama na kufanya Wilaya
ya Ilala kuwa salama. Alieleza kuwa juhudi hizo zilifanikiwa kuzuia uharibifu
zaidi wa mali za watu na mchakato wa uchaguzi.
"Tunavipongeza vyombo vya
ulinzi na usalama kwa kuokoa baadhi ya mali na kuwakimbiza wale watenda maovu
waliodhamiria kuteketeza mali za watu na kuharibu uchaguzi.
Hawakufanikiwa," alisisitiza.
Alibainisha kuwa utendaji kazi wa
vyombo hivyo ulikuwa wa hali ya juu na umehakikisha amani inarejea haraka.
Pamoja na pongezi hizo, Mkuu huyo
wa Wilaya alitoa wito kwa watendaji wa serikali na wananchi kutoa ushirikiano
wa kutosha kwa vyombo vya usalama ili waweze kuendelea na kazi ya kuwatafuta na
kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika na vurugu hizo.
"Vyombo vya ulinzi na
usalama vinaendelea na kazi. Naomba watendaji kutoa ushirikiano wa kutosha kwa
vyombo vya usalama kutoa ushirikiano. Tunataka kuhakikisha wale wote
walioshiriki katika uharibifu wanabainika."
Akitoa maelekezo ya moja kwa
moja, DC Mpogolo alimpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Elihuruma
Mabelyana kwa kutoa agizo la kuharakisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu
yote ya utoaji huduma ya umma iliyoharibiwa wakati wa vurugu.
"Nampongeza Mkurugenzi wa
Halmashauri,kwa kuelekeza miradi yote ya serikali, ofisi zote za serikali
ziendelee kujengwa na nyingine kukarabatiwa kwa ajili ya kurejesha huduma za
umma ... ile miradi yote ya serikali, ofisi zote za serikali ziendelee kujengwa
ili wananchi waendelee kupata huduma," alieleza.

0 Maoni