WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa jana Oktoba 23, 2025 amekagua ujenzi wa kituo cha Polisi
Nandagala, Ruangwa mkoani Lindi na kuagiza kituo hicho kianze kazi ifikapo
Novemba 1 mwaka huu.
Aidha,
Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa
Frank Chonya kuhakikisha samani zinawekwa katika kituo hicho ili kiweze
kutumika kwa kutoa huduma kwa Wakazi wa Wilaya ya Ruangwa.
“Wananchi
hawa wanataka kituo hichi kianze kazi, majengo yamekamilika bado viti tu,
hatuwezi kurudi kumdai IGP, Mkurugenzi simamia tupate viti hapa, pamoja na
kuweka paving katika eneo hili, malengo yetu Novemba 1 mwaka huu kituo kianze
kazi.”
Kwa
Upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, John
Imori, amesema kuwa kiasi cha shilingi
milioni 164 kilitengwa kwa ajili ya kujenga kituo cha Polisi cha daraja C,
lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza kituo hicho kijengwe kwa mfumo wa force
account na fedha nyingine zijenge nyumba za Maafisa wa Polisi.
“Tunakupongeza
sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, maagizo yako ya kujenga kwa mfumo wa force account
yametuwezesha sasa tumepata na nyumba mbili za Maafisa wa Polisi, katika fedha
ile milioni 164 tuliongeza shilingi milioni 30 tu hadi kukamilisha majengo haya
matatu.”
Ujenzi wa
kituo hicho ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 194.3 umefikia asilimia 95 za utekelezaji, kukamilika kwake
kutawezesha wananchi katika vijiji 32 kwenye kata 8 za Wilaya ya Ruangwa kupata
huduma.
Kadhalika,
Mheshimiwa Majaliwa alitembelea shule ya Sekondari ya Wasichana ya Liuguru
ambapo aliwaeleza wanafunzi hao kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza fursa kwa watoto wa kike
kupata elimu nchini.



0 Maoni