Katika kuwahakikishia Watanzania amani na umoja,
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, alisisitiza kauli ya
utawala kuhusu usalama nchini na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga
kura bila woga.
Akizungumza mkoani Geita, Wasira alitahadharisha
dhidi ya wale wanaoshawishi watu kutokwenda kutopiga kura na kusema:
"Hatukubali watu wachache wazuie umma kupiga kura."
Alibainisha kuwa umoja na amani ya nchi ndio msingi
wa maendeleo, na akagusa taarifa kuhusu watu wanaojaribu kuzuia zoezi la
upigaji kura:
"Nimesikia huko watu wanasema watu wasiende
kupiga kura, wako kwenye mitandao wanasema wakati Watanzania wanapiga kura wao
wataandamana," alisema Wasira, huku akisisitiza kwamba tarehe ya uchaguzi
ni siku ya kupiga kura na "hakuna kuandamana wala mtoto wa maandamano,
hamna."
Akithibitisha mamlaka ya serikali, Wasira alirejelea
kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa hivi karibuni Dar es Salaam
akizungumza viwanja vya Leders katika kampeni za CCM:
"Kama alivyosema Rais (Dk. Samia Suluhu
Hassan), juzi, alipokuwa anazungumza Dar es Salaam aliwaambia yeye ndiye
Amirijeshi Mkuu, alikuwa hawatishi alikuwa anawaambia tu kwamba kuna serikali
ambayo kazi yake ni kuhakikisha amani inakuwepo," alieleza Wasira.
Makamu huyo Mwenyekiti alimalizia kwa kutoa msimamo
thabiti wa Chama Tawala, akisema Serikali na CCM "haiwezi kuruhusu
uvunjifu wa amani na kuzuia umma wa Watanzania kutumia haki ya kikatiba
kuchagua viongozi," na kwamba "Hatuwezi kuruhusu watu wachache
wanaotumiwa na watu wa nje kuleta fujo katika nchi yetu."
Alisisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kwa amani na
kuwataka wapigakura waandamane "kwenda kupiga kura hakuna mtu
atawabughudhi hata mmoja, hamna."

0 Maoni