Serikali
imezindua rasmi utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimataifa wa mazingira
ujulikanao kama “Mbinu Chanya na Jumuishi za Kukabiliana na Mabadiliko ya
Tabianchi na Kulinda Bayoanuai” (Integrated Net-Zero Nature-Positive Solutions
for Climate and Biodiversity Protection), unaolenga kuendeleza sekta ya misitu
kwa lengo la kuinua maisha ya watu.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha Kamati ya
Usimamizi wa Mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.
Hassan Abbasi, ambaye ni Mwenyekiti alisema mradi huo wenye thamani ya Dola za
Marekani milioni 38 ni uthibitisho wa kuaminiwa kwa Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mradi
huu ni ushahidi wa juhudi za Serikali katika kulinda mazingira, kuhifadhi
misitu na kuhamasisha nishati safi. Dunia inatambua uongozi wa Tanzania katika
masuala ya uchumi wa kijani ndio maana baadhi ya wadau wa Mradi huu pamoja na
Serikali yenyewe ni Mfuko wa Dunia wa Mazingira na wenzetu wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP),” alisema Dkt. Abbasi.
Mradi huo
unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Wizara ya Fedha, Tume ya Mipango, UNDP,
na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF).
Naye
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini ambaye ni Mwenyekiti Mwenza katika usimamizi wa
mradi huo, Bw. Shigeki Komatsubara, ameahidi kuwa Shirika hilo litaendelea
kushirikiana na Tanzania kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya kuendeleza miradi
inayolinda mazingira lakini na kuinua
maisha na utu wa watu.



0 Maoni