Shirika
la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limepokea ugeni kutoka nchini Italia na kufanya kikao na ili kukuza
na kuendeleza mahusiano katika sekta ya uhifadhi na utalii, kikao
kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano
KINAPA.
Kabla ya
kikao hicho cha jana, ugeni huo ulipokelewa Octoba 17, 2025 kwa kupanda mlima
Kilimanjaro kupitia Lango la Umbwe kwa siku sita na kushuka jana tarehe
22/10/2025 na kushikia lango la Mweka, huku wakijionea vivutio mbalimbali
vilivyoko katika mlima huo mrefu kuliko yote duniani kama mlima uliosimama peke
yake.
Mbali na
shauku yao ya kufika katika kilele cha Uhuru chenye historia ya Taifa letu kwa
kupandishwa Bendera ya Taifa na Mwenge wa Uhuru kwa mara ya kwanza Disemba 09,
1961, wageni hao kutoka Italia pia walijikita kutoa elimu ya uhifadhi kupitia
kampeni yao iitwayo "SAVE THE MOUNTAINS" ili kuendelea kuhifadhi tunu
ya mlima huu.
Akiwakaribisha
wageni hao Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi
Maria Kirombo aliwapongeza kwa hatua hiyo inayolenga kuhifadhi Mlima Kilimanjaro
kwa manufaa ya Tanzania na dunia kwa ujumla.
Aidha
Kamishna Kirombo aliongeza,
"Watalii
wanapopanda mlima huu, wengi wao huona mazingira na kutusaidia kutoa maoni
yanayotusaidia katika uhifadhi husasani wanaokuja na kampeni kama hii ya “SAVE
THE MOUNTAIN AND THEIR CULTURAL HARITAGE” na wengine huungana na jamii
inayozunguka hifadhi kwa kupanda miti, sanjari na hilo pia mlima huu ni chanzo
cha ajira na kipato kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.”
Naye,
Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro - Afisa Mhifadhi Mkuu Amri Mtekanga
alisisitiza kuwa uhusiano huu usiishie katika zoezi la upandaji wa mlima pekee
bali uwe chanzo cha kuibua fursa za uwekezaji na kubadilishana ujuzi wa
kiteknolojia unaorahisisha upatikanaji wa mahitaji muhimu hifadhini hususani
kwa wapandaji wa mlima pamoja na elimu ya kutosha juu ya tiba na uokoaji pindi
dharura inapojitokeza.
Kwa
Upande wake Balozi wa Hiari, Bi. Judith Mushi amepongeza serikali ya Tanzania
kwa kusaidia mchakato huu kufanikiwa kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Italia
kutoa ushirikiano tangu miaka miwili iliyopita alisema, "Nia kubwa ya sisi
kuwa hapa ni kufungua milango ya mahusiano na ushirikiano katika uhifadhi na
utalii wa milima tukianza na Mlima Kilimanjaro kisha baadae kwenda kwenye
maeneo mengine".
Aidha,
kiongozi wa msafara huo Bw. Pablo Valoti aliainisha maeneo ambayo Hifadhi ya
Taifa Kilimanjaro inaweza kushirikiana na Chama hicho ili kulinda mazingira
yake ni pamoja na kukuza utalii ikiwemo mradi wa uchimbaji maji, mradi wa
kudhibiti taka kutoka kwa wageni pamoja na kutoa nafasi za elimu kwa njia ya
ufadhili wa masomo ili kwenda kujifunza kwa nadharia na vitendo vile wanachama
wanavyofanya katika utunzaji wa milima.
Sambamba
na hilo naye, Ndg. Dario Nisoli alikabidhi barua yenye jumbe anuai ikiwemo ya
kuwakaribisha watumishi wa TANAPA kutembelea nchini Italia kujifunza mambo
mbalimbali ya uhifadhi na mwendelezo wa sekta ya utalii na kupanua wigo wa
ushirikiano baina ya hizo nchi mbili.
Na.
Calvin Katera - Kilimanjaro




0 Maoni