Wakati dunia inashuhudia ongezeko la maandamano na
migomo ya vijana waliokata tamaa kutokana na ukosefu wa ajira, Serikali ya
Awamu ya Sita imeandika ukurasa mpya wa matumaini kwa kutangaza zaidi ya nafasi
40,000 za ajira katika sekta mbalimbali.
Tukielekea Uchaguzi Mkuu, ni muhimu kutambua kwamba
ajira hizi si "geresha" (za kuwavutia wapiga kura), bali ni
mwendelezo halisi wa utekelezaji wa ahadi mbalimbali za Serikali kwa wananchi
wake, zikisimamia misingi ya Kazi na Utu.
Wakati mataifa mengine yakikabiliwa na janga la
ukosefu wa ajira kama vile Afrika Kusini yenye zaidi ya 43% au Ulaya zaidi ya
25% Tanzania inaendelea kujenga matumaini kwa kuongeza bajeti ya ajira katika
Mwaka wa Fedha 2025/26. Huu ni ushahidi wa dhati wa Serikali kuleta fursa na
ustawi kwa vijana.
UPOTOSHAJI WA
MITANDAONI
Tunasikitishwa na kauli za kukatisha tamaa kutoka
kwa watu wachache kwenye mitandao ya kijamii wanaodai ajira hizi ni
"geresha." Ukweli ni mmoja: Ajira hizi ni halisi, zimetangazwa rasmi
kupitia Ajira Portal, na tayari maelfu ya Watanzania wameitwa kwenye usaili.
Kauli kama hizi si tu zinaua matumaini ya vijana, bali pia zinavuruga ari ya
Taifa.
Ajira ni Neema, Si Hadithi za Mitandaoni: Hadithi ya
Damas Mhagama, aliyeajiriwa baada ya uthubutu na uvumilivu licha ya changamoto
za kiufundi, inathibitisha kuwa mafanikio hayaji kwa malalamiko bali kwa
kuchukua hatua.
Chagua Kazi Badala ya Maneno: Kila tangazo la kazi
ni mwaliko wa kubadili maisha yako. Tumia kifurushi chako cha intaneti kutafuta
taarifa za ajira, mafunzo, na fursa za ujasiriamali, badala ya kusambaza upotoshaji
na vichekesho visivyo na tija.
Ajira ni zaidi ya kipato; ni jukwaa la kujijenga,
kujitegemea, na kujenga Taifa lenye uchumi wa kizalendo ambalo linabakia salama
na tulivu ili kuendeleza maendeleo haya.

0 Maoni