Serikali
imetoa hati za hakimiliki za kimila 580 kwa wananchi wa Kijiji cha Makibo, Kata
ya Nyahua, Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora kupitia Mradi wa Usimamizi
Shirikishi wa Misitu ya Miombo (DSL-IP), unaoratibiwa na Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS), ili kuimarisha usalama wa milki za ardhi na kupunguza
migogoro kati ya jamii na mamlaka za uhifadhi.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo jana, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Thomas
Myinga, alisema hati hizo zitawawezesha wananchi kuwekeza katika shughuli
endelevu za kilimo, ufugaji na biashara za mazao ya misitu, hatua
itakayochochea uchumi wa kaya na kulinda mazingira.
“Mipango
hii na hati hizi ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi, kupunguza upotevu wa bioanuwai na uharibifu wa ardhi. Tunataka kuona
jamii zikiwekeza katika matumizi bora ya ardhi na uhifadhi wa misitu ya
miombo,” alisema Myinga.
Kwa
upande wake, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Dkt. Zainab Bungwa,
alisema mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 6.8 (sawa na Sh
bilioni 16.8) unatekelezwa kwa miaka mitano (2023–2027) katika wilaya za
Kaliua, Urambo na Sikonge (Tabora) na Mlele (Katavi) kwa lengo la kurejesha
uoto wa asili, kupunguza uharibifu wa ardhi na kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema
mradi huo unahusisha nchi 11 ikiwamo Tanzania, Kenya, Malawi, Zimbabwe na
Angola, na umeanza kwa kutambua vikundi vya wazalishaji wa misitu na mashamba
(FFPOs) ili kuviwezesha kushiriki katika shughuli za uhifadhi na biashara
endelevu.
Dkt.
Bungwa aliongeza kuwa TFS inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo
vya ulinzi wa misitu (Ranger Posts), matumizi ya ndege zisizo na rubani
(drones) kwa ulinzi, ujenzi wa nyumba za nyuki, maghala ya mbegu na miundombinu
ya maji kwa ajili ya jamii zinazoshiriki uhifadhi.
Kwa
upande wake, Obed Katonge kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi
alisema tume itaendelea kushirikiana na mamlaka za upangaji ili kuhakikisha
ardhi inapangwa, kupimwa na kumilikishwa kwa wananchi, huku akisisitiza
wananchi kulinda hati zao na kuepuka kuazimishana, kwani kufanya hivyo
ni kuvunja sheria.




0 Maoni