Kwa mara ya kwanza katika historia ya karibuni ya
uchaguzi, wakuu wa vyombo vya habari na wahariri wameungana na kutoa azimio la
pamoja, wakihimiza wananchi wote kutanguliza amani na utulivu kabla na baada ya uchaguzi mkuu. Azimio hili
linaambatana na wito wa kukataa "uwenda wazimu wa halaiki" unaoweza
kutumiwa na wachache kubomoa misingi ya kitaifa iliyojengwa kwa miaka mingi.
Wadau hao wanasisitiza kwamba njia pekee ya kulinda
amani na kujenga taifa imara ni kupitia ushiriki mkubwa na wa amani wa wananchi
katika zoezi la upigaji kura.
Azimio hilo linasisitiza kuwa uchaguzi ni daraja la
kuimarisha demokrasia, na si uwanja wa vita.
"Ushiriki mkubwa wa wananchi huimarisha misingi
ya demokrasia nchini. Ni haki yako ya msingi ya kikatiba. Kwa kutekeleza haki
hii, unasaidia kujenga utawala bora ambapo sauti ya kila mwananchi
inathaminiwa," inasema sehemu ya azimio hilo.
Vyombo vya habari vinawahimiza Watanzania kuchukua
hatua hii kama fursa ya kutumia haki yao ya kikatiba badala ya kutoa nafasi kwa
vurugu au uchochezi. Kupiga kura kwa amani ni kuzuia kabisa jaribio lolote la
kuharibu utulivu wa nchi.
Kataa Kubomoa Misingi ya Kitaifa
Wahariri wameeleza wasiwasi wao kuhusu baadhi ya
sauti zinazoweza kutumika kusukuma ajenda ya uvunjifu wa amani kwa maslahi
binafsi.
"Tunawaomba wananchi wasikubali kuingia katika
uwenda wazimu wa halaiki na kubomoa misingi ya kitaifa. Kila mmoja wetu ana
wajibu wa kuwa Balozi wa Amani kuanzia kituo cha kupigia kura hadi anaporudi
nyumbani," inahimiza taarifa hiyo.
Vyombo vya habari vimeahidi kuendelea kutoa taarifa
sahihi na za kuelimisha, huku vikisisitiza kwamba utawala bora unajengwa na
wananchi wenye utashi wa kwenda kwenye sanduku la kura. Kila mpiga kura
anapaswa kujitambua kuwa yeye ni sehemu ya ulinzi wa amani ya nchi.

0 Maoni