Wito
umetolewa kwa vijana ifikapo Oktoba 29, 2025 kujitokeza katika vituo vya
kupigia kura na kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kuchagua viongozi kuanzia
ngazi ya Urais, Wabunge na Madiwani ambao watashirikiana pamoja katika
kuwaletea maendeleo.
Hayo
yamebainishwa na Bi. Jenista Mhagama, Mgombea wa Ubunge katika Jimbo la
Peramiho (Ruvuma) kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana Oktoba 25, 2025 wakati
aliposhiriki kwenye Bonanza la Afya, wilaya ya Songea vIjijini llilofanyika
katika uwanja wa Tamasha, Peramiho.
“Tunapoelekea
tarehe 29, 2025 bonanza letu limebeba ujumbe maalum, ikiwemo kuhamasisha vijana
wote katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, kujitokeza kwenye vituo vya
kupigia kura kutekeleza wajibu wao wa kikatiba,” amesema Bi. Mhagama.
Amesema
kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea vijana wapo wengi, hivyo kupitia
bonanza hilo amewataka kufikisha ujumbe huo kwa vijana wengi zaidi ili waweze
kutambua umuhimu wa zoezi lililo mbele yao.
“Tumekumbushana kuwa katika Jimbo la Peramiho sisi ni watu wa
amani, tumezoea kuwa na amani na tunatamani kuwa ni chachu ya amani katika
maeneo mengine yote,” amesisitiza Bi. Mhagama na kuwataka vijana kuwa mabalozi
wa amani na kutoa taarifa yeyote ya viashiria vya uvunjivu wa amani.
Bi.Mhagama
amewataka wananchi kupitia imani zao kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili
Taifa liendelee kuwa na amani na kuvuka salama katika kipindi hiki cha uchaguzi
na kupata Viongozi bora watakao waletea
maendeleo wananchi.



0 Maoni