Linda Mustakabali Wetu, Kataa Uchafuzi – Sanduku la Kura Ndiyo Jibu

 

Katika kipindi hiki muhimu sana kinachoelekea Uchaguzi Mkuu tarehe 29 Oktoba, kumetokea kauli kali, za uchochezi, na zenye kutaka kuvuruga amani kupitia mitandao ya kijamii, zikijaribu kushawishi wananchi kukata tamaa na kutumia njia zisizo za kikatiba.

Kufuatia matamko hayo yanayolenga kuingiza taifa katika machafuko, viongozi wa kitaifa, wadau wa amani, na vyombo vya habari vimekuwa vikitoa wito wa dharura: Wajibu wa Kulinda Amani ya Taifa uko mikononi mwa kila Mtanzania!

Amani Kwanza, Mustakabali Kwanza

Wakati tunatambua kuna hisia za kutoridhika na mchakato wa uchaguzi kwa baadhi ya wananchi, tunasisitiza kuwa suluhisho la changamoto za kisiasa halipatikani kwenye vurugu, machafuko, au ‘uwenda wazimu wa halaiki,’ bali kwenye utulivu na busara.

"Amani yetu ni urithi tuliopewa, hatuwezi kuutupa kwa ajili ya hisia za muda mfupi. Uchaguzi ni mustakabali wa nchi yetu. Tunawahimiza wananchi wote, bila kujali hisia zao, kuonyesha ukomavu kwa kufanya maamuzi yenye tija na kwenda kupiga kura kwa amani," anasema Mchambuzi wa Siasa na Amani Vivian Gabriel.

Sanduku la Kura Ndiye Hakimu Mkuu

Hoja ya kwamba uchaguzi unakosa maana au kwamba kura haina nguvu, inapingana na misingi ya demokrasia yenyewe. Mabadiliko ya kweli huanzia kwenye uamuzi wa kila mwananchi katika kituo cha kupigia kura.

Nini Wajibu Wako?

Piga Kura, Kataa Machafuko: Kura ndiyo njia pekee ya kisheria na kikatiba ya kuweka viongozi wanaowajibika. Kukataa kupiga kura, au kufuata wito wa kuingia kwenye fujo, ni kujisalimisha kwa watu wanaotaka kuona nchi ikiingia katika mgogoro.

Thamini Busara: Baada ya uchaguzi, bila kujali matokeo, nchi nzima itahitaji utulivu ili kujitathmini na kuendelea kujenga. Machafuko hayataleta ripoti unayotaka wala hayataleta dawa hospitalini. Yataleta maafa ambayo yatazuia maendeleo kwa miaka mingi.

Kataa Vurugu za Mitaani: Wito wa "kutukutana barabara kuu" ni mtego wa kutaka kuingiza taifa kwenye machafuko. Amani ya nchi ni ya thamani kuliko malengo ya kisiasa ya mtu binafsi au kikundi chochote. Njia sahihi ya kuonyesha kutokukubali inapaswa kufuata utaratibu wa kisheria.

Katika mahojiano mbalimbali Vyombo vya usalama vimehimizwa kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote anayeeneza ujumbe unaokusudia kuvuruga amani na utulivu. Tanzania lazima iendelee kuwa kisiwa cha amani.

Tarehe 29 Oktoba ni siku ya kutekeleza wajibu wa Kikatiba, si Siku ya Kuteketeza Taifa!

Wananchi popote walipo iwe Bunju, Kariakoo, Temeke, Mbagala, na maeneo mengine yote nchini kutafakari kwa kina na kuchagua amani. Nenda kapige kura, onyesha ukomavu wa kisiasa, na epusha nchi kuingia katika machafuko.

Chapisha Maoni

0 Maoni