Wananchi wa vijiji vya Nyantugutu, Lung'wa na
Nding'ho vya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu wameipongeza Serikali kwa kuunda
na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa taarifa
za wanyamapori wakali na
waharibifu (Problem animal information
system- PAIS) ambao umerahisisha malipo ya kifuta jasho/machozi pindi
madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu yanapotokea kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji cha
Ndi'hgo , Bi. Salome Kambona katika mkutano wa hadhara wa kuelimisha wananchi
namna ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu
uliofanyika kijiji cha Ndi'hgo ,Wilaya ya Itilima leo Oktoba 9, 2025.
"Tunaishukuru Serikali kwa mfumo huu ambao
ndani ya siku saba mwananchi atatakiwa awe ametoa taarifa ya madhara
yaliyotokana na mnyamapori ili aweze kulipwa" amesema Bi.Salome.
Naye, Mkazi wa Kijiji cha Nyantugutu, Bw. Mosses
Saguda amesema mfumo wa PAIS umepunguza urasimu na usumbufu wa malipo.
"Tunaishukuru Serikali kwa utaratibu mpya wa
mfumo wa malipo ya kifuta jasho/machozi kwani hauna usumbufu wowote na
tunalipwa kwa simu au benki tofauti na awali tulikuwa tunakaa mwaka bila
kulipwa," amesema Bw. Saguda.
Aidha, ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuweka
utaratibu wa malipo ya kifuta jasho kwa wananchi wanaoharibiwa mazao yakiwa
ghalani.
Akizungumza kuhusu elimu hiyo kwa wananchi, Afisa
Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Nassoro Wawa amesema matarajio ya
Serikali baada ya mafunzo hayo ni kwamba wananchi wamepata uelewa jinsi ya
kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kujua sheria, kanuni
na taratibu za kufuata ili kumiliki nyara za Serikali.
"Pia nimewaeleza wananchi kuwa sheria zinaruhusu kuwekeza katika sekta
ya wanyamapori hususan kuanzisha bucha za nyamapori, bustani, mashamba na
ranchi za wanyamapori ili waweze kujipatia vipato," amesisitiza Bw. Wawa.
Elimu hiyo imetolewa Mkoani humo kufuatia matukio ya
wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo,fisi,
mamba na viboko.



0 Maoni