Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani
Pwani wameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ujenzi
wa barabara ya Ruvu-Milo yenye urefu wa Kilomita 11 iliyojengwa kwa kiwango cha
changarawe.
Akiongea kwa niaba ya wananchi hao, Mwenyekiti wa
kijiji cha Kitonga, Bw. Mohamed Mtulia ameipongeza Serikali kupitia TARURA kwa
kutekeleza mradi huo ambao umeondoa vikwazo katika barabara hiyo kwani sasa
wananchi wanazifikia huduma mbalimbali za kijamii kwa urahisi.
Kwaupande wake, Bw. Yohana Underson mkazi wa kijiji
cha Milo ameipongeza TARURA kwa kutekeleza mradi huo na kwamba hapo awali
changamoto ya barabara hiyo ilikuwa kubwa hasa kipindi cha masika.
Akielezea juu ya utekelezaji wa mradi huo, Msimamizi
wa mradi kutoka TARURA wilaya ya Bagamoyo, Mhandisi Benard Mwita amesema kwa
upande wa eneo la Ruvu tayari wamekamilisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha
changarawe kilomita 11 uliohusisha pia kuinua tuta la barabara na kujenga boksi
kalavati tatu.
Ameeleza kuwa mradi huo umewanufaisha wananchi
hususani katika vijiji vya Kitonga, Milo na Migude.
"Awali eneo hili lilikuwa halipitiki kutokana
na kujaa maji lakini kwa ujio wa mradi huu sasa barabara inapitika na wananchi
wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi na Kijamii", amesema Mhandisi
Mwita.
Ujenzi wa barabara hiyo umetekelezwa kupitia mradi
wa RISE programu ya uondoaji vikwazo katika barabara (Bottleneck) kwa mkopo
nafuu toka Benki ya Dunia.



0 Maoni