Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri
Mbibo, ameongoza kikao cha wataalam kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kwa
ajili ya kujadili mikakati ya kudhibiti utoroshaji wa madini nchini.
Kikao hicho kimefanyika Oktoba 7, 2025, katika
Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Madini Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbibo amesema kuwa
ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali za
taifa, hasa madini, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
"Utoroshaji wa madini ni tishio kwa uchumi na
usalama wa taifa letu. Tunapaswa kushirikiana kwa dhati katika kudhibiti mianya
yote inayochangia vitendo hivi," amesema Mbibo.
Aidha, amesema kuwa utoroshaji wa madini umekuwa
ukiliingizia taifa hasara kubwa ya mapato, na kwamba ipo haja ya dharura ya
kuunganisha nguvu za pamoja katika kudhibiti vitendo hivyo haramu.
“Madini ni miongoni mwa rasilimali muhimu
zinazotegemewa katika kuchochea maendeleo ya taifa letu. Hatuwezi kukubali
kuendelea kupoteza mapato kwa sababu ya mianya ya utoroshaji. Ni wajibu wa kila
mmoja wetu kama watanzania wazalendo
kushiriki katika vita hii,” amesema Mbibo.
Katika kikao hicho, Mbibo ameeleza kuwa Serikali
inahitaji kuwa na mfumo thabiti na shirikishi wa udhibiti wa madini kuanzia
migodini, kwenye vituo vya ukaguzi, hadi viwanja vya ndege, bandari na mipaka
yote ya nchi.
Pia, ametoa wito wa kuundwa kwa timu maalum za
kitaifa zenye wataalam kutoka taasisi mbalimbali, zitakazoshirikiana katika
kufanya uchunguzi, ufuatiliaji na ulinzi wa madini, hasa katika maeneo ambayo
yameonekana kuwa na mianya mikubwa ya utoroshaji.
“Tunapaswa kuwekeza katika vifaa vya kisasa vya
kuchunguza na kubaini madini hususan madini ya vito kwa haraka na kwa uhakika. Vifaa hivi
vitasaidia sana kuzuia mbinu mpya zinazotumiwa na wanaojihusisha na
utoroshaji,” amesisitiza.
Mbibo pia amependekeza kuanzishwa kwa mpango wa
mafunzo endelevu kwa wataalam wanaofanya kazi katika maeneo ya ukaguzi ili
kuwajengea uwezo wa kutambua aina mbalimbali za madini, mbinu za usafirishaji
haramu na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kudhibiti biashara hiyo
haramu.
Katika hitimisho la kikao, wadau walikubaliana
kuweka mikakati ya haraka ya utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa, ikiwa ni
pamoja na kuandaa mpango kazi wa pamoja utakaohakikisha udhibiti wa utoroshaji
wa madini unafanyika kwa ufanisi na kwa muda mrefu.
Kikao hicho kimehusisha ushiriki wa taasisi
mbalimbali za Serikali ikiwemo Wizara ya Madini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi, Tume ya Madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege (TAA).



0 Maoni