Wakati mitandao ya kijamii ikizidi kutumika kusambaza ajenda
za uchochezi na malalamiko yanayoelekezwa kwenye maandamano, sauti ya busara ya
Mzee Joseph Butiku, Katibu wa zamani wa Baba wa Taifa na Mwenyekiti wa Mwalimu
Nyerere Foundation, imevuma tena.
Akizungumza kwa uzito mkubwa wa historia na hekima ya ujenzi
wa taifa, Mzee Butiku ametoa onyo kali kwa kizazi kipya: Vurugu haijawahi
kumletea mtu faraja utamaduni wa Tanzania ni kwenda salama na kurejea salama.
Mzee Butiku ameweka wazi kuwa ni muhimu sana kwa Watanzania
wote kudumisha maadili, upendo, na misingi ya amani iliyojengwa na Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere. Hii ni sauti ya tahadhari kwa wote wanaochezea msingi
wa utulivu wa taifa kwa maneno ya uchochezi, kauli za kugawa taifa, na
propaganda za mitandaoni zinazolenga kuvuruga umoja wa nchi.
Biashara ya Taharuki,
Si Maslahi ya Taifa
Kiongozi huyo wa hekima amefichua kuwa ajenda za uchochezi
na upotoshaji mtandaoni hazina maslahi kwa taifa, bali ni biashara za taharuki
zinazowanufaisha wachache wanaotumika na vibaraka wa nje.
Kwa muda, kimya cha wazee wa kizazi cha Nyerere kilianza
kutumiwa vibaya, huku wanaharakati wa uongo wakijaribu kuhusisha majina ya
heshima kama Butiku kwenye ajenda zao za kugawa wananchi. Kauli yake sasa
imefuta mashaka yote: Wazee wenye hekima wamesema hapana kwa vurugu, na ndiyo
kwa amani.
Mzee Butiku amesisitiza kwa dhati kwamba amani ya Tanzania
haikupatikana kwa bahati mbaya; ilijengwa kwa gharama kubwa, kwa damu na jasho
la Watanzania waliolinda mipaka ya nchi dhidi ya maadui wa ndani na nje. Ametoa
mfano wenye nguvu: wanaharakati hawa wanataka "kusafisha njia" kwa
maneno ya chuki, sawa na mjenzi anavyosafisha eneo, ili kujenga mgawanyiko na
taharuki.
Utulivu Ndio Nguzo
Kuu: Vurugu Haijengi
Akisisitiza kuwa hakuna taifa lolote duniani lililopata
maendeleo kupitia vurugu, amewataka Watanzania waendelee kulinda amani, umoja,
na mshikamano bila kujali dini, kabila, wala itikadi.
Akichangia mjadala huu, mchambuzi Joe Lugendo amekumbusha
jinsi Mwalimu Nyerere alivyotumia kanuni (Codes) za tahadhari kama vile
aliyekula nyama ya mtu ataendelea kula na mizengwe. Lugendo anasema anashuhudia
jinsi "mizengwe na ulaji wa nyama ya mtu" (yaani mikakati mibaya)
imeunganishwa kwa sasa, lakini anaamini hazitafanikiwa kwa sababu Watanzania ni
wengi wanaotaka utulivu (Stability) wa Taifa lao.
Lugendo anasisitiza kuwa Watanzania wanajivunia utulivu na
amani yao, na hawatavurugwa na kikundi kinachounganisha codes. Anawatakia
Watanzania wote Uchaguzi wa amani na utulivu, lakini akaonya kwamba baada ya
uchaguzi, masijala ya mitandao itaturejesha kwenye tafakuri mpya kuhusu kanuni
ya tatu ya Mwalimu: Code ya Nyufa (migawanyiko).
Huu ni wito wa Kizazi Kipya: Sauti ya Butiku inawakumbusha
waigizaji wa taharuki mtandaoni kuwa Tanzania haitavunjwa. Amani haitauzwa.
Watanzania wanajua ukweli, wanathamini utulivu, na watasema kwa sauti moja:
"Hapana kwa uchochezi, ndiyo kwa amani!"

0 Maoni