Tanzania inakabiliwa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ikiwa imara na yenye matumaini makubwa, kinyume na picha inayoanza kuchorwa na baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa, Msemaji Mkuu wa Serikali anasema akitaka kupuuzwa kwa kauli gombanishi zinazotengenezwa na waandisahi mitandaoni na mashirika ya kimataifa.
Anasema uchaguzi huu sio tishio; bali ni uthibitisho wa uimara wa taifa lililokomaa kisiasa.
"Hiki ni kipindi cha hekima, si jazba. Uhuru wa maoni haupaswi kutumika kama kisingizio cha kuchochea vurugu au kupandikiza hofu. Demokrasia ya kweli inajengwa kwa hoja, heshima, na majadiliano ya kistaarabu," anasema Gerson Msigwa katika mahojiano.
Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya Oktoba 29, ni muhimu kwa vyombo vya habari vya ndani na nje kufahamu wajibu wao: kuandika ukweli, si kuunda simulizi za hofu. Wananchi wanahitaji taarifa sahihi za kuwasaidia kufanya maamuzi, si propaganda za kuleta taharuki, anasema.
Tahadhari kwa Vyombo vya Kimataifa: Tanzania Haina "Taharuki"
Taarifa kama ile ya Deutsche Welle (DW) yenye kichwa cha habari kinachouliza “Siku 23 Kabla ya Kura Tanzania: Tumaini au Taharuki?” ni mfano wa wazi wa upotoshaji unaopuuzia uhalisia wa nchi.
Wachambuzi wa masuala ya ndani wanasema inashangaza kuona vyombo vya nje vikijifanya kuijua Tanzania kuliko Watanzania wenyewe, na kupeleka maswali ya kiasili ambayo hayapo kwa lengo la kuchochea taharuki.
Ukweli ni kwamba, Tanzania leo ni nchi ya matumaini, si taharuki, anaandika Lawrence Luwanda mwenyeji wa Mwarazi, Movomero katika mtandao wa kijamii.
Uchaguzi wa Tanzania unafanyika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi makini wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameimarisha misingi ya demokrasia na utulivu. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inatekeleza majukumu yake kwa uwazi, na ushiriki wa vyama 18 kwenye ngazi ya Ubunge na Udiwani, huku vyama 17 vikiwa na wagombea urais, ni ishara ya wazi kwamba demokrasia yetu ni imara na shindani.
Maendeleo ni Ushahidi
wa Utulivu
Tangu mwaka 2021, Serikali ya Awamu ya Sita imeandika historia mpya katika uongozi unaoelekea kwenye uchumi na diplomasia imara kwani ukuaji wa uchumi umeongezeka kutoka asilimia 5.1 mwaka 2021 hadi asilimia 7.5 mwaka 2024; ajira mpya 33,212 zimepatikana mwaka 2025 pekee katika sekta za elimu, afya, na huduma nyingine muhimu.
Aidha katika kuonesha uimara wa Tanzania, uhusiano wake kimataifa umeimarika, wawekezaji wapya wameongezeka, na mikopo ya maendeleo inaendelea kutolewa kwa masharti nafuu. Pia kuna uhuru wa vyombo vya habari na maoni umepanuka, huku mijadala ya kisiasa ikiendelea kwa uwazi bila hofu.
"Haya yote yanathibitisha jambo moja: Tanzania ipo imara, ina matumaini, na ina dira. Vyombo vya habari vya kimataifa vinatakiwa kuelewa kuwa Uchaguzi wetu ni uthibitisho wa kukomaa kwa taifa, si fursa ya kuunda hadithi za kutisha," anasema Msigwa.
Tunapoelekea Oktoba 29, kila Mtanzania ana jukumu moja: kuitumia kura yake kuimarisha demokrasia, kudumisha amani, na kujenga taifa lenye mshikamano.
Msigwa amewataka watanzania wasikubali kuchezewa akili na simulizi za hofu zisizokuwepo.
0 Maoni