Tofauti na
maneno matupu au hisia za mitandaoni, kura ndio kitendo pekee chenye mamlaka
halisi ya kuamua hatima ya Taifa.
Kama Baba
Askofu Paulo Bendera, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Dar es Salaam,
alivyoshauri, kila mmoja anapaswa kwenda kupiga kura na kumchagua anayemtaka,
kwani kususia kura ni sawa na kuchagua hewa yaani, kukabidhi uamuzi wako kwa
wengine.
Viongozi
mbalimbali wa jamii wameungana katika wito huu wa amani na utekelezaji wa haki
ya kikatiba. Mufti wa Tanzania, ambaye pia ni Shehe Mkuu wa Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (BAKWATA), Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally amesisitiza suala la
amani na kuwaambia vijana wapige kura kama njia ya kuamua hatima yao na kisha
warejee katika maeneo yao.
Mufti Zubeir
alibainisha kuwa amani ni msingi wa Uislamu, na kila Mwislamu anapaswa kuitetea
amani hiyo popote atakapokuwepo.
Kwa upande
wake, Joseph Muruta alisisitiza kuwa siasa za amani ni fahari kwa nchi yetu.
Naibu Katibu Mkuu wa Kamati ya Amani, Alhajj Othmani Mkambaku, alisisitiza
umuhimu wa kura kama haki ya kimsingi na wajibu wa kikatiba.
Alisema,
"Lazima Oktoba 29 nijitokeze, ni wajibu wangu kupiga kura kumchagua
kiongozi ninayempenda ili aweze kusimamia mambo yetu katika kipindi cha miaka
mitano."
Kizazi Kipya:
Kura Ni Matokeo, Siyo Jazba
Zikiwa
zimesalia siku chache kufikia Uchaguzi Mkuu, kizazi kipya (waliozaliwa baada ya
mwaka 2000) kiko tayari kuandika historia yake ya kidemokrasia. Hiki ni kizazi
kinachotumia teknolojia kuchambua hoja na kujua ilani, na kura kwao si tukio la
kisiasa, bali ni jukumu la kizazi.
Kupiga kura
kwa vijana hawa ni ahadi ya kulinda maendeleo, amani, na heshima ya taifa.
Wanajua kuwa siasa za maneno matupu au uvurugaji wa mitandao hauwezi
kubadilisha hali halisi. Uhalisia unaonekana katika maboresho ya huduma za
afya, elimu, na miundombinu—mambo ambayo yanawapa hamasa ya kushiriki.
Kizazi kipya
kinajua kwamba kura si kelele; ni matokeo. Ni uamuzi wa kuendeleza
yaliyojengwa, kuimarisha yanayobadilisha maisha, na kulinda urithi wa amani wa
Tanzania. Taifa hili limejengwa kwenye msingi wa majadiliano, hekima, na umoja.
Wale wanaotamani taharuki nje ya mipaka watasubiri bure, kwani Tanzania imara
haijengwi kwa fujo, bali kwa umoja wa fikra na sauti za wananchi wake.
Kizazi kipya
cha wapiga kura kimeamua. Kitaandika historia kwa kura, si kwa vurugu. Kura zao
ni sauti za matumaini, zikiongoza Tanzania katika zama mpya za amani, kazi, na uelewa.

0 Maoni