Uwekezaji uliofanywa na serikali ndani na nje ya
nchi umeongezeka kwa asilimia 7 hadi kufikia Sh92.29 trilioni Juni 30, 2025
kutoka Sh86.3 trilioni katika mwaka wa fedha 2023/24.
Uwekezaji huu wa serikali unahusisha mashirika ya
umma 255 na kampuni 45 ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache, na taasisi
za kigeni 10, ambazo kwa pamoja zinatengeneza uti wa mgongo wa mapato yasiyo ya
kodi ya Tanzania.
Katika kipindi cha miaka mitano uwekezaji wa ndani
umeongezeka kutoka Sh 67.01 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh90.61 trilioni mwaka
2024/25, jambo linalodhihirisha utendaji bora na usimamizi ulioboreshwa katika
mashirika ya umma.
Hilo limeenda sambamba na kukua kwa thamani ya
uwekezaji wa serikali katika taasisi za nje ambao ulitoka Sh 722.94 bilioni
hadi Sh 1.68 trilioni.
Takwimu hizi zinazopatikana kwenye Taarifa ya
Msajili wa Hazina ya mwaka ulioishia Juni 30, 2025, zinaeleza kuwa ukuaji huo
umetokana na utendaji bora wa mashirika muhimu ya umma na ufanisi katika
uendeshaji wa taasisi mbalimbali.
Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema
ongezeko hilo linaonyesha juhudi endelevu za serikali katika kuimarisha
usimamizi na utawala bora wa uwekezaji wa umma.
“Ukuaji huu wa uwekezaji unaonesha maboresho katika
utawala wa mashirika umma, uhusiano wake na malengo ya maendeleo ya taifa,”
alisema Bw. Mchechu.
Kwa mujibu wake, mashirika makubwa kadhaa
yamechangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la mtaji wa serikali.
Kwa mfano Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
ulirekodi ongezeko la asilimia 29 katika mali halisi, kutoka Sh7.2 trilioni
hadi Sh9.3 trilioni.
Kichocheo kikubwa ni uandikishaji wa wanachama wapya
kutoka sekta isiyo rasmi na ujumuishaji na mifumo mingine ya serikali kama
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA).
Sanjari na NSSF, Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa
Umma (PSSSF) ulionesha ongezeko la asilimia 13 katika mali halisi, kutoka
Sh8.12 trilioni hadi Sh 9.2 trilioni.
Ukuaji huu ulichochewa zaidi na kuongezeka kwa
michango ya wanachama kufuatia ajira mpya na vyeo kwa watumishi wa umma.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pia iliripoti ongezeko
kubwa la mali halisi lililokuwa kwa asilimia 82
kutoka Sh1.3 trilioni hadi Sh2.36 trilioni ikiwa ni matokeo ya utendaji
thabiti wa kifedha na usimamizi mzuri wa akiba.
Bw. Mchechu alisema ongezeko la jumla la uwekezaji
wa serikali limechangiwa pia na taarifa za kifedha zilizoboreshwa ambazo sasa
zinaonesha thamani halisi ya hisa na mitaji ya serikali.
“Tumeona pia ongezeko la akiba na faida zilizokusanywa katika mashirika
kadhaa, sambamba na kuongezeka kwa faida katika mashirika mengi ya umma,”
aliongeza.
Hata hivyo, kwa baadhi ya mashirika hasa yale
yaliyoko kwenye hatua za maendeleo kama kampuni za madini yalishuhudia kupungua
kwa mtaji kutokana na matumizi makubwa ya uwekezaji na kuwa na mapato madogo.
Kwa ujumla, uwekezaji wa serikali unatawaliwa zaidi
na mashirika yasiyo ya kibiashara, ambayo yanabeba asilimia 72 ya uwekezaji wa Sh65.44
trilioni, ikilinganishwa na Sh25.17 trilioni (asilimia 28) zilizowekezwa katika
mashirika ya kibiashara.
Mapato yasiyo ya kodi yaongezeka
Utendaji mzuri wa mashirika ya umma haukuinua tu
thamani ya uwekezaji wa serikali bali pia uliongeza ukusanyaji wa mapato yasiyo
ya kodi.
Taarifa ya OMH inaonyesha kuwapo kwa ongezeko la
asilimia 34 katika mapato yasiyo ya kodi kutoka Sh767 bilioni mwaka 2023/24
hadi Sh1.03 trilioni mwaka 2024/25.
Ukuaji huo ni sawa na asilimia 92 ya lengo la mwaka
huku faida kubwa na nidhamu bora ya kifedha katika mashirika ya umma zikitajwa
kuwa sababu za ufanisi.
Asilimia 92.01 ya makusanyo ilitokana na gawio, na
michango (inayokokotolewa kama asilimia 15 ya mapato ghafi), huku kiasi
kilichobaki kikitokana na marejesho ya mikopo, faida za ziada na mfumo wa TTMS
(Telecommunications Traffic Monitoring System).
Hiyo ikiwa na maana kuwa ofisi ilifanikiwa kukusanya
zaidi ya asilimia 50 ya lengo kwa michango, gawio na marejesho ya mikopo.
Wakati huo, marejesho ya ziada na TTMS yalifikia
asilimia 44 na 37 ya malengo yao husika, mtawalia.
“Utendaji bora wa kifedha wa mashirika ya umma
umeongeza mapato kwa serikali, jambo linaloimarisha dhamira yetu ya kupunguza
utegemezi wa mapato ya kodi na kukuza fedha endelevu kwa miradi ya maendeleo,”
alisema Msajili wa Hazina.
Bw Mchechu aliongeza kuwa serikali itaendelea
kuhakikisha ukuaji endelevu wa uwekezaji wake kupitia mageuzi, ufuatiliaji wa
karibu na uwajibikaji mkubwa wa mashirika ya umma.
“Ukuaji huu ni ushahidi wa maendeleo tunayoyapata
katika kuhakikisha uwekezaji wa umma unaleta thamani kwa wananchi,” alisema.
“OMH itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi
mbalimbali kuboresha utendaji, uwazi na mchango wa mashirika ya umma katika uchumi
wa taifa.”
Agosti 24, 2025 Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango
alipokiwa akizungumza katika uzinduzi wa Mkutano wa Wakuu wa Taasisi na
Wenyeviti wa Bodi (CEOs Forum 2025) alisema mageuzi katika taasisi za umma si
hiari bali ni wajibu kutokana na uwekezaji mkubwa wa serikali katika taasisi
hizo.
“Utawala bora wa taasisi za umma ni ajenda kuu ya
serikali ili kuhakikisha uwekezaji huu mkubwa unaleta matokeo halisi kwa taifa,
taasisi hizi lazima zitoe huduma bora, zikuze ajira, na zichangie kwa kiasi
kikubwa mapato ya taifa,” alinukuliwa.
Uwekezaji wa nje
Uwekezaji wa serikali katika taasisi kumi za nje
ulipanda kwa kasi, kufikia Sh1.68 trilioni kufikia Juni 30, 2025 sawa na
ongezeko la asilimia 98 kutoka Sh846.22 bilioni mwaka uliopita.
Ukuaji huu umetokana na mabadiliko ya viwango vya
ubadilishaji wa fedha, akiba zilizokusanywa na faida za uendeshaji
katika taasisi muhimu.
0 Maoni