Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe. Zacharia
Mwansasu, Oktoba 8, 2025 amefunga rasmi
mafunzo siku 10 ya kukabiliana na ghasia (Anti-Riot) kwa kikosi maalum cha
Askari 60 wa mwitikio wa haraka wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania
- TAWA (RRT) katika Kituo cha Mafunzo cha Welela Mkoani Njombe, akisisitiza
umuhimu wa nidhamu, weledi na uzingatiaji wa sheria katika utekelezaji wa
majukumu ya uhifadhi.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mhe.
Mwansasu alisema "Serikali inatambua changamoto zinazowakabili Askari wa
Uhifadhi, ikiwemo hatari wanazokutana nazo katika kulinda rasilimali za taifa,
ambapo baadhi wamejeruhiwa na wengine kupoteza maisha." Na kuongeza kuwa
mafunzo hayo yaliyotolewa na TAWA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi
yatasaidia kuongeza ufanisi na uwezo wa askari kukabiliana na ghasia kwa
kutumia nguvu ya kadiri bila kuathiri haki za binadamu.
Mhe. Mwansasu alieleza kuridhishwa na umahiri
uliooneshwa na Askari hao katika mafunzo ya vitendo, yakiwemo matumizi ya
mabomu ya machozi, upekuzi, ukamataji watuhumiwa na mazoezi ya ukakamavu.
Alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kutoa mafunzo hayo na kuomba kuendeleza
ushirikiano huo ili kuboresha utendaji wa Jeshi la Uhifadhi.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alitumia fursa hiyo
kulaani vikali vitendo vya baadhi ya wananchi kuvamia na kuwashambulia Askari
wa Uhifadhi wakiwa kazini. Aliwataka wananchi kuacha mara moja kufanya shughuli
za kibinadamu ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuheshimu sheria za uhifadhi.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Mwansasu aliipongeza
Menejimenti ya TAWA kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwataka wahitimu kutumia ujuzi
walioupata kuboresha uhifadhi na kuongeza mapato kupitia utalii.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi – Huduma
za Shirika, Thabit Maarufu, ambaye alimwakilisha Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa
TAWA, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na
Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha TAWA kifedha na kwa
rasilimali watu, jambo linalozidi kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa
majukumu ya uhifadhi nchini.
Aidha, Naibu Kamishna Maarufu alitoa shukrani kwa
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, kwa kuruhusu wataalamu wa
jeshi hilo kushiriki katika kutoa mafunzo ya kukabiliana na ghasia kwa Askari
wa Uhifadhi. Alisema ushirikiano huo ni kielelezo cha mshikamano wa taasisi za
ulinzi na usalama katika kulinda rasilimali za taifa.
Akizungumzia mipango ya mbele, alibainisha kuwa TAWA
imeandaa mpango maalumu wa kuboresha mfumo wa mafunzo kwa kuongeza kozi
mbalimbali ikiwemo mafunzo ya uokoaji majini na kuogelea kwa askari wake, ili
kuwaongezea uwezo wa kukabiliana na changamoto katika maeneo mbalimbali ya
uhifadhi.
Vilevile, alisema mamlaka imepanga kuongeza vifaa,
kuboresha miundombinu ya mafunzo, na kuhakikisha Kituo cha Mafunzo cha Welela
kinajengewa uwezo wa kuwa kituo bora na cha mfano nchini katika kutoa mafunzo
ya kiusalama na uhifadhi.
Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa
TAWA, Abraham Jullu, amelishukuru Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori Duniani
(WCS) Kwa mchango wake mkubwa linalotoa Katika shughuli za uhifadhi nchini
hususani uwezeshaji wa mafunzo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya RRT yanayolenga kuimarisha uwezo na umahiri wa
Askari hao katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi.
Aidha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Asel
Mwampamba aliishukuru TAWA kwa kutambua mchango wa Jeshi la Polisi katika kutoa
mafunzo hayo, akisisitiza kuwa ushirikiano huo utaendelea kuimarisha nidhamu,
ufanisi, na weledi katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi nchini.
Kadhalika, Mratibu wa ulinzi wa program ya Ruaha
Katavi WCS Bw. Stanley Mbilinyi alisema
Shirika hilo linajivunia kushirikiana kwa ukaribu na TAWA katika kuanzisha na
kuunga mkono vikosi vya kwanza vya RRT nchini Tanzania tangu mwaka 2015, pamoja
na kushirikiana na taasisi hiyo kuandaa
nyaraka muhimu za mipango na kujenga uwezo wa kutekeleza
mbinu hii kitaifa.
Na. Beatus Maganja - Njombe
0 Maoni