Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua Mradi wa Dunia
wa kukabiliana na magonjwa ya Mlipuko nchini na kuzitaka wizara zote tawala za
mikoa na serikali za mitaa pamoja na taasisi kutekeleza shughuli za kipaumbele
katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na dharura za kiafya.
Dkt.
Biteko ametoa agizo hilo Oktoba 15, 2025 jijini Mwanza na kusema mradi huo
wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 38.7 unalenga kuboresha huduma za
afya kwa watanzania na kuchochea maendeleo ya nchi.
Amesisitiza
kuwa wizara, taasisi na washirika wa maendeleo wanatakiwa kusimamia utekelezaji
katika uwekezaji huo na kuhakikisha yanapatikana matokeo chanya kama
ilivyokusudiwa.
“Wizara
zote, Tawala za mikoa na Taasisi , tekelezeni shughuli zote za kipaumbele
katika kukabiliana na magonjwa haya ya mlipuko na dharura nyingine za afya
kulingana na maeneo yenu na hakikisha kwamba hakuna hata shilingi moja
inayopotea au kuchepushwa kando ya malengo yaliyokusudiwa,” amesema Dkt.
Biteko.
Amesema
kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na wadau wote wa ndani na
nje ya nchi kuimairsha mradi huo ili uweze kuleta matokeo chanya katika
kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa tishio kwa maisha ya watu na
kurudisha nyuma maendeleo.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu,
Mhe. Ummy Nderiananga amesema uzinduzi wa mradi huo, ni muhimu katika jitihaza
za kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Amesema
mradi huo unatekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia sehemu ya Afya moja
pamoja na wadau wa maendeleo likiwemo Shirika la Afya Duniani(WHO), Shirika la
Umoja wa mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Chakula na Kilimo
(FAO) na Pandemic Fund.
Kwa
upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya ambaye ni Mganga Mkuu wa Serikali,
Dkt. Grace Magembe amesema mradi huo utaboresha mwitikio wa mifumo ya afya
katika kukabiliana na magonjwa kama Ebola, MPOX, Marburg, ZIKA na magonjwa
mengine yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Dkt.
Magembe amefafanua kuwa utekelezaji madhubuti utawezesha upatikanaji wa taarifa
za haraka kuhusu uwepo au uvumi kuhusu magonjwa ya mlipuko na hivyo kuzifanyia
kazi taarifa hizo.
Amesema
upatikanaji wa fedha hizo utawezesha pia maboresho ya maabara ya taifa na
kikanda ikiwa ni njia ya kupata taarifa za haraka kwa usahihi kutoka kwa
wananchi.
Akizungumzia
utekelezaji wa mpango huo, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt.
Salim Nassor Slim amewashukuru viongozi wa Kitaifa kwa hatua za kuboresha afya
za wananchi ili kuwa na afya bora.
Naye
Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNICEF, Dkt. Patricia Safi ameipongeza Tanzania kwa
ushirikiano ulipo kati yake na mashirika ya kimataifa na kuongeza kuwa Shirika
hilo litahakikisha linaendeleza mashirikiano katika kutatua changamoto za
kijamii.
Amesema
UNICEF itahakikisha mchango wake unajikita katika maendeleo ya mtoto na kufanya
jitihada za kuwezesha watoto wote wanapata huduma kwa mujibu wa mipango
iliyopo.
Na. Ofisi
ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati




0 Maoni