Mahakama
Kuu Masjala Kuu jijini Dodoma leo imeitupilia mbali kesi iliyofunguliwa na
Luhaga Mpina pamoja na chama chake cha ACT-Wazalendo wakipinga kuenguliwa kwake
kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Katika
uamuzi uliotolewa leo Jumatano, Oktoba 15, 2025, mbele ya jopo la majaji
watatu, Mahakama hiyo imesisitiza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania pamoja na sheria zilizopo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
(INEC) haiwezi kuingiliwa na chombo chochote kwa maamuzi inayoyafanya ikiwa
imeyafanya kwa nia njema na ndani ya mipaka ya kisheria.
Akisoma
uamuzi huo, Jaji Fredrick Manyanda ambaye alikuwa kiongozi wa jopo hilo,
alisema kuwa hoja zilizowasilishwa na upande wa walalamikaji hazikutosha
kuiamuru INEC kubadili uamuzi wake wa kumengua Mpina. Majaji wengine waliokuwa
katika jopo hilo ni Sylvester Kainda na Abdallah Gonzi.
Kwa
uamuzi huo, Luhaga Mpina hatashiriki rasmi katika kinyang’anyiro cha urais,
ambacho tayari vyama mbalimbali vya siasa viko katika harakati za kampeni
kuelekea siku ya kupiga kura.
Mpina,
aliyekuwa mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo, alikuwa amefungua kesi hiyo
akiitaka Mahakama Kuu itengue uamuzi wa INEC uliomwengua kwa madai ya kukiuka
baadhi ya masharti ya uteuzi.

0 Maoni