Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imejibu ripoti ya shirika la
kimataifa la haki za binadamu, Amnesty International, kuelezea wasiwasi wake
mkubwa kuhusu lugha na aina ya madai yaliyomo katika ripoti hiyo.
Katika majibu yake, Serikali imesema, ingawa
Tanzania iko wazi kwa ushirikiano na
washirika wa kimataifa, inasikitisha kuwa Amnesty International ilichagua
kuchapisha muhtasari uliojaa madai makubwa na yasiyokuwa na uthibitisho bila
kuipa Serikali fursa ya kutosha kujibu kabla ya kuachia ripoti hiyo.
Serikali imesisitiza kuwa mbinu kama hiyo inahujumu kanuni
za ukweli na kuheshimiana ambazo zinapaswa kuongoza mazungumzo ya kimataifa
kuhusu haki za binadamu.
Taarifa hiyo ya serikali imesema kwamba katika miaka
yote imejikita katika ulinzi na kukuza haki za binadamu, kama ilivyohakikishiwa
na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (kama
ilivyorekebishwa). Ulinzi huo unalingana na mikataba ya kimataifa na kikanda ya
haki za binadamu ambayo Tanzania inatii, ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki
za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.
Serikali imekataa maelezo ya ripoti hiyo kuwa
Tanzania ni nchi isiyoonea haya ukamataji holela, kupotezwa kwa lazima, na
kukandamizwa kwa uhuru wa kujieleza. na badala yake Tanzania inatekeleza sera
ya kutovumilia kabisa mateso na aina nyingine za unyanyasaji wa kikatili na
usio wa kibinadamu.
Aidha imesema madai ya yab kuwapo kwa uhalifu
huchunguzwa na mamlaka husika kama vile Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora (CHRAGG), Kurugenzi ya Mashtaka ya Umma (DPP), na Mahakama, sambamba na
sheria za Nchi.
Serikali imeeleza wazi kuwa haitoi msamaha kwa
matukio ya kupotezwa au mauaji ya kiholela. Kila tukio linaloripotiwa linapaswa
kuchunguzwa kwa kina na kupatiwa suluhisho la kisheria, huku Mahakama
ikiendelea kuwa huru na kuhakikisha watu wote wanapata dhamana ya kesi za haki
chini ya sheria za ndani na za kimataifa.
Serikali imesisitiza zaidi kwamba uhuru wa
kujieleza, kukusanyika kwa amani, na upatikanaji wa taarifa unalindwa na Katiba
na kudhibitiwa kupitia sheria kama vile Sheria ya Huduma za Habari na Kanuni za
Maudhui Mtandaoni. Sheria hizi zinatekelezwa kulingana na Kifungu cha 19(3) cha
ICCPR, ambacho huruhusu vikwazo vidogo vinavyohitajika ili kulinda usalama wa
taifa, utulivu wa umma, na haki za wengine.
Mchakato wa Uchaguzi:
Kuhusu uchaguzi, Serikali imedai kuwa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi (INEC) inafanya kazi kwa uhuru kama inavyohakikishwa na
Katiba. Tanzania itaendelea kuwezesha uangalizi wa uchaguzi na kudumisha kanuni
za uwazi, kutopendelea, na usawa katika kushiriki siasa.
Katika taarifa hiyo Serikali imehitimisha kwa
kusisitiza tena dhamira yake katika utawala wa kidemokrasia, utawala wa sheria,
na ulinzi wa haki za binadamu, kabla, wakati, na baada ya Uchaguzi Mkuu wa
2025. Imesisitiza kuwa iko wazi kwa majadiliano na wadau wote na inahimiza
taasisi zote kuwasiliana moja kwa moja na mamlaka husika kabla ya kuchapisha
taarifa zinazopotosha umma.

0 Maoni