HALMASHAURI
ya Manispaa ya Mpanda na Mkandarasi M/s Chonqing International Construction
Corporation (CICO), wametiliana saini mkataba wa ujenzi wa barabara za kiwango
cha lami zenye urefu wa Kilomita 8.4.
Makubaliano
hayo ya mradi huo wa Uendelezaji
Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC), yanajumuisha ujenzi wa barabara 10 kwa
kiwango cha lami, ujenzi wa jengo la usimamizi wa mradi na magari manne ya kusimamia
utekelezaji wa mradi.
Makubaliano
hayo yamefikiwa leo Oktoba 25, 2025 katika halfa iliyofanyika mjini Mpanda
mbele ya mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko.
Akizungumzia
utekelezaji wa mradi huo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mjini (TARURA) Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC, Mhandisi
Emmanuel Manyanga, amesema mradi huo utatekelezwa kwa miezi 15 kuanzia Novemba
Mosi, 2025.
“Ujenzi
wa miundombinu hii utahusisha barabara za Mkumbo Junction – Nsemulwa Health
Center (Km 1.68), Nsemulwa Health Center – Sokoine (Km 1.23) Kapufi (Mita 760,
Sumry (Mita 460), Pinda (Mita 260) Fimbo ya Mnyonge (Mita 390) Fish Market
(Mita 330), Mpanda Hotel (Mita 760), Mikocheni Junction – White Gireffe (Km
1.88) na Homeground (Mita 730),” amesema Manyanga.
Mhandisi
Manyanga amesema mradi huo utasimamiwa na Mshauri Elekezi M/s NIB Plan Consult
Limited kutoka Dar es Salaam.
Aidha,
ameeleza kuwa mradio wa TACTIC utagharamia pia kuandaa mipango kabambe (Master
Plans) kwa miji 19 iliyo chini ya Mradi huo.
"Pamoja
na uboreshaji wa miundombinu, pia mradi huu una kipengele cha kujengea uwezo
taasisi zote za Wizara, TARURA pamoja na Halmashauri za Miji kupitia mafunzo
mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji kazi, ufanisi wa huduma mbalimbali
kwa jamii pamoja na kununua vitendea kazi kama vile magari ya usimamizi na
ufuatiliaji, pamoja na kuhuisha mifumo ya ukusanyaji mapato,” amesisitiza
Mhandisi Manyanga.
Kwa
upande mwingine wananchi wa Mkoa huo,
wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo ambao utaboresha mandhari ya
mji huo na kukuza uchumi wa wananchi wake.
Mwenyekiti
wa Baraza la Wazee Mkoa huo, Vicent Longino Nkana, ameishukuru Serikali
inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa inayoendelea kufanya
hasa ya kuboresha miji ambayo hapo awali ilikuwa mapori na mingine haina mvuto.
"Dkt.
Samia amefanya kazi nzuri sana ya kutuletea wananchi maendeleo kama mradi huu
kwenye mji wetu, ametufaa sana na tunamshukuru kwa kazi kubwa anayoendelea
kufanya,” amesema Nkana.
Aidha,
ameiomba TARURA kuwajengea barabara nyingine za mji huo ili kuendelea kuunganisha
na kukuza uchumi wa wananchi hao.
Mradi wa
TACTIC ni mojawapo ya miradi inayofadhiliwa na Serikali kuu kupitia mkopo wa
Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 410 (Bila VAT).
Malengo
ya mradi huu ni kuboresha miundombinu ya Miji 45 ya Tanzania pamoja na kujengea
uwezo taasisi (Halmashauri) ili ziweze kujiimarisha katika usimamizi wa
uendelezaji miji pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Lengo kuu
la mradi wa TACTIC ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji pamoja na
kuziwezesha Halmashauri za Miji na Majiji kutoa huduma
bora kwa wananchi.


0 Maoni